UCHAFU WAZAGAA TENA JIJINI DAR ES SALAAM

Takataka  zimezidi kuzagaa katika jiji la Dar es Salaam na kuna maeneo ambako hazijazolewa kwa zaidi ya wiki mbili.
Maeneo hayo ni Kariakoo, Jangwani, kituo cha daladala cha Tabata kilichopo barabara ya Mandela, kituo cha treni cha Mabibo, Mabibo sokoni,  Manzese, Buguruni sokoni, Bunju, Boko, Mwananyamala, Kinondoni na  Mbweni.
Utafiti uliofanywa na mwandishi kwa wiki nzima, umebaini taka nyingi zimelundikana katika maeneo hayo bila kuzolewa kwa muda mrefu.
Taka hizo zinatoa harufu kali na nzi wamejazana kila mahali, hivyo kuleta kero kwa wananchi.
Wakazi wa maeneo hayo waliohojiwa na mwandishi, walishutumu viongozi wa Manispaa za Kinondoni na Ilala kwa kuzembea hadi kusababisha kero hiyo.
Aidha, walidai juhudi zilizoanzishwa na Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadiki na Mkurugenzi wa Jiji, Wilson Kabwe za kusafisha jiji, zimezorota hivi sasa, kwani hawasikiki tena wakihimiza suala hilo.
Aidha, waliwashutumu wabunge wa Dar es Salaam na viongozi wa serikali za mitaa, kwa kufumbia macho uchafu, ulioanza kujazana tena mitaani na barabarani.
Wengine walilaumu makandarasi waliopewa zabuni ya kuzoa taka, kwa madai hawaonekani mitaani na pia viwango wanavyotozwa ni vikubwa mno.
Wazoaji taka hao wanadaiwa kutoza kati ya Sh 10,000 na 30,000 kwa kila nyumba,  kiwango ambacho ni kikubwa na wananchi wengi wa kawaida hawawezi kumudu.
Mkazi wa mtaa wa Kariakoo kata ya Kariakoo, Hafsa Jumanne alisema wanalazimishwa kulipa ada ya uzoaji taka ya Sh 15,000 kwa madai wapo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
“Nashangaa waraka wa Manispaa ya Ilala unasema ada ya uzoaji taka iwe kati ya Sh 5,000 na 10,000 sasa wao wamezidisha na kwa sasa tuna karibu wiki mbili taka hazijazolewa”, alisema.
Mkazi wa Mbweni Teta wilayani Kinondoni, Zuhura Makwaia alisema wanatozwa Sh 30,000 kwa mwezi kama ada ya uzoaji taka na Kampuni ya Sumaita.
“Wanatutoza Sh 30,000 kwa mwezi na wanakuja kuchukua taka mara moja kwa wiki ambayo ni Alhamisi, wengine hawana uwezo wa kulipa, wanalazimika kuchimba mashimo ndani ya nyumba zao au kutupa kwenye viwanja vya watu ambavyo havijajengwa nyumba,” alisema.
Hata hivyo, mwandishi alipopiga simu kwenye Kampuni hiyo ya uzoaji taka kwa kutumia simu ilizoandika kwenye gari lao la uzoaji taka, lilielezwa ada ni Sh 30,000 kwa mwezi na wanachukua mara moja kwa wiki.
Alipoulizwa kuhusiana na kulundikana kwa taka hizo, Msemaji wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Muhowera alisema hiyo imetokana na wakandarasi wengi kushindwa kuzoa kwa sababu wananchi wanakwepa kulipa ushuru wa taka.
“Wananchi wanachelewa kulipa taka, unakuta mtu analipa Januari na hadi Julai hajalipa. Jukumu hili si la serikali peke yake bali ni la wananchi na serikali za mitaa,” alisema.
Alisema ada hiyo inaanzia Sh 1,000 hadi 2,000 kwa maeneo ya wakazi wenye hali za chini kama Tandale na maeneo yaliyopitishwa kutozwa ada kubwa ni Mikocheni na Msasani ambayo ni kati ya Sh 10,000 na 15,000.
“Si kweli Mbweni wanatozwa Sh 30,000 kwanza haiwezekani kutozwa bei hiyo ingawa bei zinapangwa na serikali za mtaa kwa wananchi na watendaji baada ya kufanya sensa ya nyumba na kiasi cha taka, umbali wa kupeleka takataka dampo la Pugu Kinyamwezi  kisha wanagawana kiasi cha fedha lakini hakuna eneo lililozidi Sh 15,000”, alisema.
Alipoulizwa Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira Manispaa ya Ilala, Charles Wambura alisema viwango vya uzoaji wa taka ni kati ya Sh 10,000 na 15,000 na kwa wasio na uwezo wameruhusiwa kutozwa Sh 5,000.
Alisema ucheleweshaji wa kuzoa taka unatokana na ucheleweshaji wa ulipaji wa ada hivyo wakandarasi wanashindwa kuzoa taka na wasiolipa ada hizo ndiyo wanaoanzisha malalamiko. Pia kuna upungufu wa magari ya kuzoa taka.

No comments: