SERIKALI YAFUTIA VIWANDA VIBALI VYA MAGOGO, KUNI

Serikali imesitisha vibali vyote vilivyotolewa kununua kuni na magogo kwa ajili ya nishati ya kuendesha viwanda mbalimbali nchini na badala yake imevitaka ndani ya muda wa miezi mitatu kuanzia jana viwe vinatumia teknolojia ya makaa ya mawe, umeme na gesi kwa ajili ya kuviendesha viwanda vyao.
Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira juzi, Dk Binilith Mahenge baada ya kufanya ziara katika kiwanda cha kufuma nguo cha Sunflag kilichopo eneo la Themi, jijini hapa na kushitushwa na shehena kubwa ya magogo yaliyorundikwa kiwandani hapo ambayo hutumika kama nishati.
Kutokana na hali hiyo, Dk Mahenge amefuta vibali vyote  vilivyotolewa kwa kiwanda hicho na vingine vya kununulia kuni kwa ajili ya nishati, huku ikipigwa faini ya Sh milioni 80 na pia kuamriwa kupanda miti milioni saba ili kufidia uharibifu.
Aidha, uongozi wa kiwanda hicho umetakiwa kuhakikisha unawalipa walinzi watakaowekwa na serikali ngazi ya mkoa ili kuzuia uingizwaji wa magogo na kuni  kiwandani hapo kwa ajili ya nishati.
Waziri alikitoza faini hiyo kutokana na uharibifu mkubwa wa  mazingira na kuagiza kuwepo na ushirikiano kati ya uongozi wa mkoa na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) Kanda ya Kaskazini kutafuta eneo litakalopandwa miti milioni saba na kiwanda hicho ili kufidia uharibifu.
Waziri huyo wa Mazingira ambaye pia ni mbunge wa Makete mkoani Njombe amesisitiza kuwa matumizi ya nishati ya magogo katika uendeshaji maboila katika kiwanda umepitwa na wakati kutokana na mabadiliko ya teknolojia.
Kwa upande wake mwanasheria wa NEMC, Manchale Heche alisema kutokana na shehena kubwa ya miti iliyovunwa na kiwanda hicho uongozi wa kiwanda hicho unapaswa kupanda zaidi ya miti milioni saba ili kufidia uharibifu huo. Alisisitiza kwamba kiwanda hiki kimechangia mabadiliko makubwa katika mfumo wa  hali ya hewa.

No comments: