RAIS KIKWETE AONGOZA MAADHIMISHO KUMBUKUMBU YA MASHUJAA

Rais Jakaya Kikwete jana aliongoza maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa huku viongozi wa dini walioongoza dua wakiombea Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba watakaporudi bungeni kuweka uzalendo na maslahi ya taifa mbele.
Rais Kikwete aliwasili kwenye Mnara wa Mashujaa uliopo katika Bustani ya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam saa tatu asubuhi akiambatana na Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange na kisha wimbo wa taifa ulipigwa, kisha Kikundi cha Buruji chenye Askari sita wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania kilitoa heshima, ikifuatiwa na mizinga.
Mara baada ya matukio hayo, ilifuata ratiba ya kuweka silaha za jadi na mashada ya maua ambapo Rais Kikwete alianza kwa kuweka Mkuki na Ngao kwenye Mnara wa Mashujaa, akifuatiwa na Mkuu wa Majeshi Jenerali Mwamunyange aliyeweka sime, aliyefuatia alikuwa Kiongozi wa Mabalozi, ambaye ni Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Juma Mpango aliyeweka shada la maua, kisha Meya wa Jiji la Dar es Salaam Didas Massaburi aliyeweka upinde na mshale na wa mwisho alikuwa ni Mwenyekiti wa Tanzania Legion Rashid Ngonji ambaye aliweka shoka.
Ratiba iliyofuata ilikuwa ni viongozi wa dini kuomba dua kwa ajili ya Mashujaa waliojitolea na kupigania taifa pamoja na kuombea taifa hili ambapo wakizungumza walisisitiza umuhimu wa wajumbe wa Bunge maalumu la Katiba kuweka uzalendo mbele wakati wa mchakato unaoendelea wa kutafuta Katiba Mpya.
Mchungaji Steven Magana kutoka Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) alimuomba Mungu wakati huu ambapo taifa liko katika mchakato wa kutafuta Katiba Mpya wajumbe watakapokuwa katika Bunge Maalumu la Katiba waweke uzalendo mbele na maslahi ya taifa.
Mmoja wa viongozi wa dini kutoka Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Liberatus Kadio alisema wakati huu ambapo mchakato wa Katiba unaendelea aliomba wajumbe wa Bunge maalum la Kariba na Watanzania kujadili kwa umakini na kuwezesha kupata Katiba itakayotoa fursa ya uhuru, nidhamu, upendo na maridhiano miongoni mwa Watanzania.
Kadio aliomba Mungu kuliepusha taifa na purukushani zozote zitakazo vuruga amani, kuliepusha na uchochezi wa kisiasa na kidini na Watanzania kuwa na roho ya Hekima ya kujali viongozi na viongozi kuwa na moyo na hekima ya kutumikia wananchi. Aliomba pia Mungu kuepusha dunia na vita na kwamba Mungu awe amani kwa Tanzania.
Kiongozi wa dini kutoka madhehebu ya Kiislamu, Shehe  Mkoyogole alisema siku ya kumbukumbu ya mashujaa ni muhimu kwani Watanzania wanakumbuka watu waliojitoa mhanga kwa ajili ya taifa hili na kwamba ni wakati kizazi cha sasa kukumbuka kuwa wapo watu wazalendo  waliotetea nchi hii.

No comments: