SUMAYE, MZEE MWINYI WAKEMEA UDINI

Rais mstaafu wa Awamu ya Pili , Ali Hassan Mwinyi ametaka Watanzania kuwa makini kwa kutoruhusu tofauti za dini zilizopo nchini, kuwa chanzo cha mgawanyiko miongoni mwao.
Wakati Mwinyi akihadharisha hayo kwenye futari iliyoandaliwa na Mkuu wa  Mkoa wa Dar es Salaam,  Said Meck Sadiki, pia Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye akiwa mkoani Arusha, amekemea chuki zinazotokana na imani za watu, akisisitiza umma kutambua kwamba vita haina macho.
Sumaye alisema hayo juzi alipokuwa akitoa salamu katika Mkutano Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati mjini Arusha.
Mwinyi alisema hayo katika futari hiyo, iliyoandaliwa kwa ajili ya  watoto wanaoishi katika vituo vya kulea yatima, wananchi na viongozi mbalimbali. Alisema kila mtanzania, bila kujali imani yake, anao wajibu wa kulinda na kutunza amani.
Mwinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo, alihimiza watanzania kuendelea kudumisha upendo na ukarimu kwa wenzake, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyomo katika vitabu vitakatifu.
“Nawasihi Watanzania wenzangu tuendelee kupendana, tuwe wamoja katika kushirikiana, kamwe tusiruhusu wala kukubali mgawanyiko wa dini wala itikadi zetu,” alisema.
Alishukuru viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa uamuzi wa kuandaa futari iliyounganisha  yatima, wananchi na viongozi wengine, bila kujadili itikadi na dini zao, ikiwa ni ishara ya kuonesha upendo na ukarimu walio nao.
Kwa upande wake, Sadiki alisema wanaendelea kutekeleza  mipango mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo  ukarabati  na ujenzi wa miundombinu iliyoharibiwa vibaya wakati wa msimu wa  mvua jijini Dar .
Akiwa kwenye mkutano huo wa KKKT, Sumaye alisema “Eneo lingine la hatari sana ni chuki za kidini au zinazotokana na imani za watu. Vita yoyote haina macho lakini vita ya kidini ni mbaya zaidi na huishia kuuana bila kuwa na mshindi. Nchi yetu hatujawa na tatizo kubwa na jambo hili lakini hatuko salama sana.”
Alisema Watanzania wakiwa na umoja, udini hauna nafasi kwa sababu hakuna dini inayofundisha chuki kwa binadamu mwenzake. Alisisitiza kila mtu ana uhuru wa kuabudu dini aitakayo, ili mradi havunji sheria za nchi.
 Hata hivyo, alisema viongozi wa dini nchini, ni chachu ya maadili mema. Katika mkutano huo uliomchagua  Mchungaji Solomon Massangwa, kuwa Askofu wa Dayosisi hiyo, kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Askofu Dk Thomas Laiser,  Sumaye alisema nchi inakabiliwa na tatizo la maadili.
Alisema tatizo linaanzia kwa vijana hadi wakubwa.  “Je katika upungufu huu wa maadili ya jamii, viongozi wa kiroho mna nafasi ipi ya kudhibiti mambo haya? Au mtasubiri makanisani na kuwaombea msamaha wale wanaotubu tu?,” alihoji.
Alisisitiza, “Ni lazima shughuli zetu za siasa zifuate sheria na taratibu zilizowekwa kwa uwazi bila kutiliwa shaka na upande wowote. Haki ni lazima isimamiwe kikamilifu nyakati zote za kampeni hadi upigaji wa kura, kuhesabu kura na hata kutangaza matokeo.”

No comments: