WALALAMIKA KUPIGWA MARUFUKU MITUMBA NGUO ZA NDANI ZANZIBAR

Wafanyabiashara wa nguo za ndani za mitumba wameilalamikia Serikali kwa kupiga marufuku uingizaji na usambazaji wa nguo hizo kwa kile walichodai umewatia hasara kubwa.
Mfanyabiashara anayeuza bidhaa za nguo za ndani za mitumba katika soko la Saateni Ali Haji, alisema uamuzi wa Serikali kupiga marufuku nguo hizo utaathiri biashara zao na kurudisha nyuma juhudi za kujiajiri katika sekta binafsi.
Haji alifafanua na kusema hadi sasa Serikali haijatoa ufafanuzi sababu za msingi za kupiga marufuku nguo hizo ikiwamo ushahidi wa madhara ya kiafya kama inavyodaiwa na Serikali.
“Nguo za ndani za mitumba zinatoka Ulaya ambapo huko nguo hizo ni salama na hazina madhara yoyote ya kiafya kama inavyodaiwa na wizara, zinapimwa na zinafaa kwa matumizi,” alisema.
Naye mfanyabiashara wa sidiria za mitumba, Iddi Haji, alisema kwa zaidi ya miaka 10 amekuwa akifanya biashara hiyo katika soko la Mwanakwerekwe.  Alisema tangu afanye biashara hiyo hajapata malalamiko ya aina yoyote kutoka kwa wateja kuwa na madhara ya kiafya.
“Mimi nafanya biashara hii kwa muda mrefu sasa, lakini sijapokea malalamiko kutoka kwa wateja ikiwemo athari za afya kwa wateja,” alisema Haji.
Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui alitangaza Serikali kupiga marufuku biashara za nguo za ndani za mitumba na kutoa muda wa miezi mitatu nguo hizo kuondoshwa katika soko la Zanzibar.
Mazrui alisema uamuzi huo ni kutekeleza sheria ya biashara nambari 4 ya mwaka 2013 ambayo inapiga marufuku matumizi ya nguo za ndani za mitumba katika soko la biashara.
Akifafanua zaidi Mazrui alizitaja bidhaa zilizopigwa marufuku kuuzwa katika soko la biashara la Zanzibar ni pamoja na soksi, magodoro pamoja na nguo za ndani.
“Serikali inatoa kipindi cha muda wa miezi mitatu biashara ya mitumba ya nguo za ndani kuondoshwa katika soko la biashara kutokana na athari za za kiafya,” alisema.
Mazrui alisema uamuzi huo wa kutekeleza sheria hiyo lengo lake kubwa kuweka mfumo mzuri wa biashara na kuweza kuwalinda watumiaji wa bidhaa hizo na madhara ya kiafya.
Alisema tayari baadhi ya nchi za Afrika ya Mashariki zimepiga marufuku uingizaji wa bidhaa hizo pamoja na biashara hiyo ikiwemo Tanzania Bara, Kenya na Uganda katika soko la ndani la wateja.

No comments: