BARABARA KUFUNGWA KUPISHA SIKUKUU YA MASHUJAA

Baadhi ya barabara za Jiji zitafungwa kwa muda kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa watu watakaohudhuria maadhimisho ya Siku ya Mashujaa kesho.
Barabara zitakazofungwa ni Lumumba, Uhuru na Bibi Titi, lengo likiwa ni kuhakikisha usalama kwa watumiaji wake na wahudhuriaji wa sherehe hizo zitakazofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini hapa.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki aliyasema hayo jana alipotembelea mazoezi yanayofanywa na wanajeshi katika viwanja hivyo. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete.
Alisema kamati ya maadhimisho hayo itaweka runinga katika maeneo muhimu ya Mnazi Mmoja kuwezesha kila mshiriki kupata fursa ya kuona vizuri matukio yanayoendelea.
"Napenda pia kuhimiza suala la usafi katika majumba yote yanayozunguka viwanja hivi vya Mnazi Mmoja kuleta taswira nzuri," alisema Sadiki.
Alisema maadhimisho hayo yataanza saa 2:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana na kuongeza kuwa ni kumbukumbu muhimu katika historia ya nchi kwani ni kuwaenzi mashujaa walijitoa katika jitihada za kuikomboa nchi na kuilinda na kudumisha amani.

No comments: