MLEMAVU ASIYE NA MIGUU AZUIA MSAFARA WA RAIS KIKWETE

Rais Jakaya Kikwete amezidi kuthibitisha moyo wake wa utu na kupenda watu hasa wahitaji, baada ya kusimamisha msafara wake, kushuka kwenye gari na kwenda kumsalimia mlemavu asiye na miguu.
Mlemavu huyo, Edwin Ngonyani (37), alikuwa akimsubiri Rais jirani na geti la nyumba anapoishi Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Tukio hilo lilivuta hisia za wengi, kwa kuwa kijana huyo alifika eneo hilo kwa kujiburuza chini muda mfupi tu kabla Rais hajaondoka eneo hilo kwenda wilayani Tunduru.
Baada ya kijana huyo kufika hapo, hakuingia ndani ya uzio, alikaa pembeni ya magari kusubiri Rais atoke, muda mfupi baadaye safari ya msafara huo ilianza, lakini mara tu gari la Rais lilipotoka nje ya uzio, magari yalisimama na Rais Kikwete alishuka.
Kiongozi huyo alikwenda alipokuwa kijana huyo, akainama, akampa mkono kumsalimu na kumuuliza maswali ili kumfahamu zaidi.
Baada ya kumsalimia, Rais Kikwete alimpa fedha kijana huyo, na kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana baadaye, alimpa Sh 200,000.
“Jana nimekuona...kwa hiyo umezaliwa hivi?” Rais alimuuliza kijana huyo anayeishi katika kijiji cha Digela, kilichopo umbali wa zaidi ya kilomita 50 kutoka mjini Namtumbo mkoani Ruvuma.
Wakati wote huo, Kikwete alikuwa ameinama kuzungumza na kijana huyo na akamuuliza kama amekuwa na ulemavu tangu kuzaliwa kwake. Kijana huyo alimjibu Rais kwamba hakuzaliwa nao, bali mwaka 2000 alipata ajali ya kuungua moto.
“Kwani huna ndugu? Unakaa na nani?” Rais alimuuliza. Ngonyani alimjibu kuwa anaishi na bibi zake na kwamba, alifika mjini Namtumbo jana yake.
Rais alimuuliza kijana huyo anafanya shughuli gani, akamjibu kwamba, hafanyi kazi yoyote.
“Basi tutakutafuta, tuone namna ya kukusaidia angalau usafiri, sasa huyu usafiri gani, au bajaj?” Aliuliza Rais Kikwete huku akionesha kuguswa na hali ya kijana huyo.
Kikwete alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu kuchukua taarifa za kijana huyo, asaidiwe na akaagiza pia Ngonyani apewe usafiri wa kurudi kwao kutoka hapo alipokuwa.
Wakati wa mkutano wa hadhara mjini Tunduru, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alisema Rais Kikwete anawapenda wananchi wake. “Rais wetu anapenda watu, ni mwenye upendo,” alisema.
Rais Kikwete aliwaeleza wananchi kwenye mkutano huo kuwa wakati anakwenda hapo, alikuta wananchi wengi njiani na asingeweza kuwapita bila kuwasalimia.
Katika sehemu nyingi alipopita, msafara wa Rais ulikuwa unasimama na kiongozi huyo aliwasalimia wananchi, kusikiliza kero zao, na kutoa ufafanuzi kuhusu namna ya kumaliza matatizo hayo.

No comments: