SONGAS, IPTL NDIO WAUZAJI PEKEE UMEME KWENYE GRIDI

Kampuni za Songas Tanzania na Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ndio  kampuni pekee za binafsi zinazozalisha umeme kwa ajili ya gridi ya Taifa.
Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja Uhusiano wa Tanesco, Adrian Severin katika mahojiano.
Alisema kutokana na hali hiyo  umeme kutoka Aggreko na Symbion Power Tanzania hutumiwa wakati wa dharura.
Alisema kuwepo kwa kampuni mbili kunatokana na  ukweli kuwa nchi kwa sasa inazalisha umeme kutoka katika vyanzo vingine vyenye gharama nafuu.
 Aidha alisema kwa sasa uzalishaji kutokana na maji na nishati ya mvuke ni megawati 752 ambayo inatosheleza mahitaji katika gridi ya taifa. Mahitaji makubwa ya umeme Tanzania mara ya mwisho yalirekodiwa kuwa megawati 898.5.
Wakati huo huo, Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL, Harbinder Sethi alisema IPTL chini ya uongozi wa Pan Africa Power Solutions (PAP) imejitoa katika hali ya kupata faida kubwa ya kupindukia, kwa kuanza kufanya uendeshaji wa gharama nafuu ikiwa na lengo la kuipatia nchi umeme wa bei nafuu.
“Ni kweli kuwa uzalishaji wa nishati kwa kutumia mafuta mazito ni ghali na ndiyo sababu tuna mpango wa kuweka mitambo ya gesi ya megawati 200 pembezoni mwa IPTL katika awamu ya kwanza ya mkakati wetu wa upanuzi. Majadiliano yanaendelea na mamlaka zote zinazohusika. Lengo ni kuhakikisha kuwa watanzania wote wanapata nishati ya bei rahisi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kuwafikia watu wengi zaidi hivi karibuni,” alisema.

No comments: