JAPAN YAONGEZA FEDHA UJENZI WA BARABARA ZA JUU

Serikali ya Japan imeongezea Tanzania Sh bilioni 5.7 kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa barabara za juu eneo la Tazara, Dar es Salaam zinazotarajia kuanza kujengwa Oktoba na Novemba mwaka huu.
Hayo yalisemwa jana na Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada wakati wa hafla ya kutia saini mkataba wa ujenzi huo jijini Dar es Salaam.
Alisema wameongeza fedha hizo kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi na ongezeko la bei ya vifaa vya ujenzi. Alisema mkataba wa makandarasi unategemewa kutiwa saini Septemba na mradi utaanza mara baada ya hatua hiyo.
Katika kuimarisha usambazaji wa umeme Dar es Salaam, tayari serikali ya Japan imetoa nyongeza ya zaidi ya Sh bilioni 70 ambazo zinahusika na ujenzi wa vituo vidogo vitano vya umeme na njia za kusambaza umeme.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Servacius Likwelile alisema anayo furaha kuona Japan imeongezea Serikali kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya mradi wa barabara ya Tazara.
Wakati huohuo, Umoja wa Ulaya (EU) umetoa magari 21 kwa ajili ya kusaidia taasisi tano zinazotekeleza mpango wa biashara na kilimo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam  jana  wakati wa kukabidhi magari hayo, Kaimu Mkuu wa ujumbe kutoka EU kwa Tanzania, Tom Vens,  alisema magari hayo ni ya Sh bilioni 1.4.
Magari hayo na taasisi zilizokabidhiwa ni ya utafiti wa kahawa (7), Bodi ya Pamba (6), maabara ya Taifa ya kusimamia ubora wa samaki (4), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) (2) na ya utafiti wa chai Tanzania (2).  

No comments: