POLISI YAAHIDI SIKUKUU TULIVU YA IDDI EL FITRI

Jeshi la Polisi nchini limejipanga kuhakikisha wananchi wanasherehekea sikukuu ya Idd el Fitr kwa amani na utulivu.
Jeshi hilo limesema kwamba limeweka mikakati thabiti ya kuimarishwa ulinzi katika maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine.
Aidha, inakusudia kuwabana madereva walevi na wazembe watakaokiuka sheria za usalama barabarani.
Hayo yameelezwa na msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso (pichani) katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuhusu mikakati ya jeshi lake katika kipindi hiki cha sikukuu za Idd el Fitr zinazoashiria kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Alisema  katika kuhakikisha usalama kwenye kumbi za starehe, wamiliki wa kumbi hizo wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi zao katika uingizaji wa watu kulingana na uwezo, badala ya  kujaza watu kupita kiasi, kwa tama ya fedha .
Aidha aliwataka wananchi wachukue tahadhari watokapo kwenye makazi yao kwa kuhakikisha hawaachi nyumba wazi ama bila mtu na watoe taarifa kwa majirani zao, na pale wanapowatilia mashaka watu wasiowafahamu.
Aliwataka  wasikae kimya bali watoe taarifa haraka kwenye vituo vya Polisi vilivyo karibu nao au kwa namba ya simu 0754 785 557, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka.

No comments: