KAYA MASKINI KUOKOLEWA NA TASAF III

Mpango wa awamu ya tatu wa Mfuko wa Maendeleo ya jamii nchini (Tasaf), unatarajia kutumia Sh bilioni 408, kwa ajili ya kunusuru kaya masikini milioni 1.2 zinazoishi kwenye hali duni, imeelezwa. 
Asilimia kubwa ya fedha hizo za Tasaf ni mkopo ikiwemo Sh bilioni 330 za Benki ya Dunia, Sh bilioni 45 zimetolewa na Serikali ya Tanzania, Sh bilioni 24 zimetolewa na Uingereza, Hispania imetoa Sh bilioni 9 na Sh bilioni 1.4 zimetolewa na Marekani.
Akizungumza juzi wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Tasaf, Ladislaus Mwamanga, Wambura alisema: “Aina ya miradi itakayotekelezwa ni ujenzi na ukarabati wa madarasa ya shule za msingi na sekondari, nyumba za walimu, vyoo, maji, ofisi za walimu, maktaba, maabara, miundombinu ya maji na mabweni”.
Alitaja miradi mingine itakayotekelezwa ni ujenzi wa madaraja ya waendao kwa miguu, karavati, umwagiliaji kwa njia ya mifereji, visima vilivyochimbwa kwa mkono, uvunaji wa maji ya mvua, ujenzi wa malambo na kilimo mseto.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Elias Ntiruhungwa alisema kutakuwa na ugumu wa kupata walengwa wa kunufaika na miradi hiyo endapo wanasiasa wataingiza itikadi zao na kuweka ndugu zao.
Alisema Serikali imejipanga kikamilifu kwa ajili ya kunufaisha kaya hizo masikini .

No comments: