LEO NI SIKU YA KULIOMBEA TAIFA

Watanzania bila kujali imani zao wameombwa kujitokeza kwa wingi leo katika maombi maalumu ya kuliombea Taifa amani, utulivu na uzalendo wa kweli na kuliepusha na vurugu na matukio ya kigaidi.
Aidha, suala la mchakato wa Katiba mpya litaombewa pia na imeelezwa kuwa, bila amani, uzalendo na amani ya kweli, maridhiano hayataweza kupatikana kwa kuwa kila upande utakuwa unajali maslahi binafsi na si ya Taifa.
Katika maombi hayo yatakayofanyika kwenye Kituo cha Sala na Maombezi cha Emaus kilichopo Ubungo kinachoratibiwa na Chama cha Kitume cha Karismatiki Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe.
Katibu wa Karismatiki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Merdad Banzi aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, maombi hayo kwa Taifa ni maalumu kuuombea mchakato wa Katiba mpya, amani na utulivu, Uchaguzi Mkuu ujao na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Banzi alisema kabla ya maombi hayo yatakayofanyika leo mchana katika viwanja vya kituo hicho cha sala kilichopo nyuma ya stendi ya mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani, pia watatembelea vituo vya watoto yatima, magereza ya Ukonga, Keko na Segerea pamoja na vituo vya wazee wasiojiweza.
Alisema pia watatembelea hospitali za Mwananyamala, Temeke, Amana,  Muhimbili na Ocean Road ambako kote huko watatoa misaada mbalimbali kulingana na mahitaji wa walengwa pamoja na kuomba nao kuwatia moyo kwamba Mungu hajawaacha na anawapenda.

No comments: