MUHONGO ADAI BEI YA UMEME TANZANIA NI YA CHINI ZAIDI

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema Tanzania ndiyo nchi pekee miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo bei ya umeme ni ya chini zaidi.
Pamoja na hali hiyo, serikali imedhamiria kuchukua hatua za kuzidi kupunguza bei ya nishati hiyo, kuwezesha umeme kupatikana kwa uhakika na kwa gharama nafuu zaidi na kwa wananchi.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Dar es Salaam juzi, ilieleza kuwa Muhongo aliyasema hayo katika mkutano wa hadhara, uliofanyika juzi mjini Mbinga. Mkutano huo baadae ulihutubiwa na Rais Jakaya Kikwete.
Mbele ya Rais na wananchi, Profesa Muhongo alisema Tanzania inauza uniti moja ya umeme kwa senti 16.8 tu za dola ya Marekani, wakati nchi nyingine za EAC zilizobakia, zinauza umeme wake kwa gharama kubwa zaidi.
Akitoa mfano, alisema Kenya inauza uniti moja kwa senti 18, Uganda inauza kwa senti 18.5 wakati Rwanda inauza umeme wake kwa senti 23 za dola ya Marekani.
Rais Kikwete na Muhongo, wote kwa nyakati tofauti katika mkutano huo  walisema kuwa pamoja na kwamba umeme wa Tanzania ni rahisi kuliko ilivyo katika nchi nyingine za Afrika Mashariki, bado Serikali inaangalia hatua ambazo zitazidi kupunguza bei hiyo ili iwe ya chini zaidi.
Kikwete alifungua pia stendi mpya na ya kisasa ya mabasi na kufungua barabara mpya ya lami ya kutoka Songea hadi mjini Mbinga.
Stendi hiyo yenye vyumba 112 vya kisasa vya kufanyia biashara, imejengwa kwa gharama ya Sh bilioni 2.17, ikiwa ni mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa (LGLB)
Akipata maelezo ya ujenzi wa barabara ya Songea-Mbinga, Rais Kikwete alielezwa kuwa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 78, imegharimu dola za Marekani milioni 64.3 na imegharimiwa na Serikali ya Marekani kupitia taasisi yake ya Millennium Challenge Corporation (MCC) na kampuni tanzu ya MMC ya Millennium Challenge Account Tanzania (MCA-T).

No comments: