IRINGA YAADHIMISHA SIKU YA CHIFU MKWAWA

Kwa mara ya kwanza Mkoa wa Iringa umeadhimisha Siku ya Kumbukumbu ya Chifu wa Wahehe, Mtwa Mkwawa tangu afariki kwa kujiua mwenyewe miaka 116 iliyopita.
Maadhimisho hayo yalifanyika juzi, ambapo ilielezwa kuwa Serikali ya Ujerumani, imerejesha jino la Mkwawa walilolichukua baada ya kubaini Chifu huyo amejiua.
Mkwawa, jemedari wa Wahehe ambaye kirefu huitwa Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga, alizaliwa mwaka 1855 na alijiua Julai 19, 1898.
Sherehe hizo za kumbukumbu ya kifo chake zilifanyika katika kijiji cha Kalenga, ilikokuwa ngome yake kuu na ambako ndiko yaliko makumbusho yake. Mkwawa aliongoza vita katika eneo lake dhidi ya wakoloni.
Wakati wa maadhimisho hayo juzi, mvua kubwa ilinyesha sehemu kubwa ya kijiji hicho, jambo lililoelezwa na baadhi ya wazee wa kimila, kwamba inaashiria furaha ya tukio hilo.
Wakati wa maadhimisho hayo, kitukuu wa Mkwawa ambaye ni Chifu wa sasa wa Wahehe, Abdul Mkwawa alitoa taarifa kuwa serikali ya Ujerumani imerejesha jino la Mtwa Mkwawa, lililochukuliwa kwenye kinywa cha Mtwa baada ya kujiua wakati wa mapambano nao.
Chifu Abdul Mkwawa alisema jino hilo limerejeshwa rasmi wiki iliyopita na mmoja wa wajukuu wa askari wa kijerumani aliyeongoza mapambano dhidi ya askari wa Mtwa Mkwawa. Walimng’oa jino kwa hasira kwa kushindwa kumuua.
Akizungumza katika sherehe hizo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliahidi kuwa serikali itaboresha makumbusho ya Mkwawa yaliyopo Kalenga yawe ya kudumu.
Pinda alisema hayo katika hotuba yake, iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Dk Binilith Mahenge.
Kwa mujibu wa muongoza wageni katika makumbusho hayo, Zuberi Suleimani, tozo ya kuona fuvu la Mkwawa lililohifadhiwa humo ni Sh 20,000 kwa mgeni kutoka nje ya nchi na wa ndani ni Sh 1,000.

No comments: