AJALI ZA BODABODA ZAMTISHA RAIS KIKWETE

Kasi ya ajali za pikipiki imemtisha Rais Jakaya Kikwete na ameeleza wasiwasi kwamba ikiendelea hivyo, utafika wakati idadi ya watu watakaokufa itakuwa kubwa kuliko wanaopoteza maisha kutokana na Ukimwi.
Rais Kikwete ameonya polisi dhidi ya ulegevu katika kukabili uvunjifu wa sheria za barabarani na amesema kwa kufanya hivyo, vifo vitaongezeka.
Ametaka wasilegee katika kuhakikisha madereva wa pikipiki na abiria wao, wanavaa kofia ngumu  kuepuka madhara makubwa zinapotokea ajali.
"Sharti lile la kuvaa kofi ya chuma kwa mwendeshaji pikipiki na abiria wake siyo urembo, ni sharti la usalama. Ndugu zangu, ajali zimekuwa nyingi mno na vifo vyake vinaongezeka kiasi cha kwamba vitapita hata vifo vinavyotokana na ukimwi," alisema Kikwete.
Alisisitiza, “Nawaomba pia ndugu zangu wa polisi wasilegeze kamba kabisa katika kukabiliana na uvunjifu wa sheria za barabara kwa sababu kwa kufanya hivyo, vifo vitaongezeka."
Rais alisema hayo wakati akihutubia mamia ya wananchi kabla ya kufungua kituo cha mabasi mjini Mbinga.
“Ajali ni nyingi, tukihesabu ajali nyingi za barabarani ni za pikipiki na si za magari,” alisema.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga alieleza katika mkutano huo kwamba wilaya hiyo ina mkakati maalumu wa kuendeleza vijana kiuchumi kwa kuwakopesha wafanye biashara waongeze vipato vyao.
Kwa mujibu Ngaga, madereva 30 wa bodaboda wilayani Mbinga wamekopeshwa sh milioni 55 ambazo kati yake, Sh milioni 18 zimetolewa na Mfuko wa Jimbo.
Mwenyekiti wa waendesha Bodaboda Mbinga, Emmanuel Ndomba ni miongoni mwa waliokopeshwa, Rais Kikwete amemkabidhi kadi ya chombo hicho cha usafiri kwa kuwa amemaliza kulipa deni.
Kabla ya Rais kumkabidhi kadi hiyo, alimuuliza  “Wewe ukiendesha pikipiki unavaa helmet? Akamjibu “ndiyo”, akamuuliza tena “Na abiria wako anavaa helmet? akamjibu “hapana”
Rais Kikwete alimwambia, “Ukiendesha pikipiki ukivaa helmet na abiria wako avae helmet…yaani huyu jamaa anajilinda yeye mwenyewe, abiria wake akifa shauri yake.”
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete ameambiwa ujenzi wa barabara za Ukanda wa Mtwara zenye urefu wa kilometa 823 kutoka mjini Mtwara hadi Mbamba Bay Mkoa wa Ruvuma, uko mbioni kukamilika.
Ili kukamilisha ujenzi wa barabara hizo,  Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alisema Serikali imetangaza dhamira yake ya kujenga kilomita 66 zilizobakia kutoka mjini Mbinga hadi Mbamba Bay, hivyo kukamilisha ujenzi wa barabara kuu za Mtwara Corridor.
Akizungumza kwenye mkutano mkubwa wa hadhara, ambao ulihutubiwa juzi na Rais Kikwete, anayeendelea na ziara ya siku sita katika Mkoa wa Ruvuma, Dk Magufuli alisema vipande vingine vya kilometa hizo 832 za Mtwara Corridor, ama vimekamilika au ujenzi unaendelea.
Alisema vipande vilivyokamilika ni Mbinga-Songea chenye urefu wa kilomita 78, Songea-Namtumbo yenye urefu wa kilometa 71.4, Mangaka-Masasi na Masasi-Mtwara ambacho lami yake ni ya siku nyingi na sasa inahitaji ukarabati.
Vipande ambazo ujenzi wake unaendelea ni Namtumbo-Matemanga chenye urefu wa kilometa 128.2, Matemanga- Tunduru chenye urefu wa kilometa 195 hadi Mangaka na hadi Mtambaswala.

No comments: