WANACHAMA 'MIZIGO' RUKSA KUONDOKA CHADEMA

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema uongozi wake, utakilinda chama kwa gharama yoyote na kuwa milango iko wazi kwa watu wasio na nia ya dhati kuondoka.
Mbowe amesema chama  kinawatakia kila la heri, wanaoondoka. Amesema wakati mwingine wamekuwa na watu mizigo, lakini wameacha mazingira yawaondoe kuliko kuwaondoa ili kutowapa sababu.
“Tunawatakiwa kila la heri waendako. Wakati mwingine unakuwa na watu mizigo kama gunia la misumari, ukiwapunguza utawapa sababu kinachotakiwa ni kuacha mazingira yawafanye waondoke wenyewe,” alisema Mbowe.
Alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu hali ya kisiasa ndani ya chama, iliyojadiliwa kwenye mkutano wa siku mbili wa Kamati Kuu ya Chadema, jijini Dar es Salaam.
“Mimi na viongozi wenzangu tutakilinda chama hiki kwa gharama yoyote na mtu yeyote awe mwanachama, awe kiongozi ambaye hayuko tayari kusimamia kwa dhati ya kweli harakati za chama milango iko wazi,” alisema.
Alisisitiza kuwa Chadema si chama cha kufuga wasaliti, wanaofanya uwakala wa vyama vingine vya siasa.
Mbowe alisema ujenzi wa chama cha siasa ni  sawa na safari ya kwenda kwa treni, ambako wapo abiria wanaoshuka na kupanda katika kila kituo.
“Siyo mara ya kwanza kutetereshwa. Ninachotaka kuwahakikishia wanachama, mashabiki na wapenzi kuwa Chadema iko imara na haitishiki na baadhi ya wanachama kujitoa,” alisisitiza.
Mbowe alisema hatua ya baadhi ya viongozi wa Chadema katika mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora, kujitoa imelenga kutoa taswira potofu ya kuwa chama kinabomoka na kuwapo kwa mgogoro.
Alisema viongozi waliojitoa, wameshindwa kuleta mabadiliko katika maeneo yao na kwamba wana hofu ya kung’olewa katika uchaguzi wa  ndani ya chama.
“ Viongozi wa Kigoma wamekuwa na Mbunge mmoja tangu mwaka 1993, na madiwani wamepungua kutoka watano hadi mmoja, na ni tofauti na NCCR-Mageuzi ambao wametoka kwenye sifuri hadi kuwa na wabunge watatu,” alisema.
Alisema kwa upande wa Tabora, wameshindwa hata kuwa na mbunge. Alisema kuondoka kwao ni nafuu kwa chama.
Wakati Mwenyekiti huyo wa Chadema akitoa kauli hiyo, juzi Kaimu Mwenyekiti na Katibu wa Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, wamekihama chama hicho na kujiunga CCM.
Licha ya viongozi hao kujiuengua, wanachama wengine wapatao 150 wamekihama, wakidai kuchoshwa na siasa zisizokuwa na tija, zinazokwamisha maendeleo jimboni Ulanga Mashariki.
Viongozi waliotangaza kuhama ni Kaimu Mwenyekiti, Zimani Marice na Katibu Deodatus Beth. Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi hao walisema wameamua  kujiunga na CCM kwa hiari yao, kutokana na utendaji mzuri wa kazi  wa Mbunge wa Ulanga Mashariki,  Celina Kombani.
 Viongozi hao walichukua uamuzi huo kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho, uliofanyika mjini  Mahenge juzi   wakati wa ziara ya Kombani, ambaye pia ni Waziri  wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Beth alisema tangu ajiunge na Chadema, amekuwa akitumia fedha zake za mfukoni kuendesha chama, bila msaada wa viongozi wa ngazi ya  juu.
Kuhusu mchakato wa katiba, Mbowe alisema hali ni tete. Alisema Chadema kitaendelea na mazungumzo ya Ukawa.
Alisema kwa sasa kumekuwa na mazungumzo ya vyama, kuangalia wanatokaje katika hali ya sasa. Hata hivyo, aliendelea kuilaumu CCM kwamba imekuwa na ajenda ya kutaka baadhi ya wabunge warejee ili kupitisha katiba wanayoitaka.
“Kuna mazungumzo ya kuangalia tunatokaje hapa, Chadema tulikwenda kwa lengo la kutafuta haki na katiba bora na si kumtafuta mshindi,” alisema.
Akizungumzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Mbowe alisema: “Hata uchaguzi ukifanyika kesho, Chadema tuko tayari na hatutasusa na tuna uhakika wa kushinda”.

No comments: