MADIWANI WAMLAUMU MKUU WA WILAYA KWA KUWADHALILISHA

Madiwani wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida waliokuwa wamewekwa mahabusu kwa amri ya Mkuu wa Wilaya, Queen Mlozi (pichani), wamesema kitendo hicho kimewadhalilisha na kuwaondolea heshima mbele ya jamii.
Madiwani hao, Hinga Mnyawi wa kata ya Ikhanoda na Ntandu Seleman wa kata ya Mwasauya, walituhumiwa kukwamisha ujenzi wa vyumba vya maabara.
Aidha, kwa nyakati tofauti mbele ya kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo juzi, madiwani hao walidai kuwa kuwekwa kwao korokoroni hakukuwa na uhalali wowote.
Akichangia kwenye taarifa ya kamati ya huduma za kijamii, Mnyawi alisema kuwa anasikitishwa mno na kitendo cha Mlozi kumweka ndani kwa kile alichodai yeye kushindwa kuhamasisha wananchi kuchangia Sh milioni 5 za ujenzi wa maabara kwenye shule iliyopo kwenye kata yake.
“Hivi ina maana mimi sijui kazi yangu hadi DC (mkuu wa wilaya) aje kunikumbusha wajibu wangu kwa kuniweka ndani?” alihoji Mnyawi.
Naye Seleman alisema kuwa anashangazwa na kitendo cha mkuu huyo kumkejeli kuwa analala Singida mjini ‘kwa raha zake’ badala ya kusaidia kusukuma mbele ujenzi wa maabara kwenye eneo lake kijijini.
Akichangia suala hilo, diwani wa kata ya Kinyeto, Francisco Ng’eni alisema kuwa kitendo cha Mlozi kuwaweka ndani madiwani wenzake ni kuwadhalilisha mbele ya jamii iliyowachagua.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Eliya Digha alihitimisha mjadala huo kwa kusema kuna umuhimu wa madiwani wa halmashauri hiyo kukutana na Mlozi kurejesha uhusiano ambao unaelekea kupotea.
Julai 8 mwaka huu, Mlozi alitumia madaraka aliyonayo kisheria kuwakamata na kuwaweka ndani kwa saa mbili madiwani wa kata hizo mbili kwa tuhuma mbalimbali, ikiwamo kushindwa kuhamasisha wananchi kuchangia ujenzi wa maabara.

No comments: