YATIMA 500 WASHEREHEKEA PAMOJA IDD EL FITRI

Zaidi ya watoto yatima 500 wanaoishi katika mazingira magumu jijini Dar es Salaam na wilayani Kondoa, Singida wameungana na Waislamu wengine duniani kusherehekea Sikukuu ya Idd el Fitr.
Sherehe hizo zilizofanyika juzi, jijini Dar es Salaam, zilitokana na kumalizika kwa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Watoto hao kutoka vituo mbalimbali vya watoto yatima, walipata fursa ya kula na kufurahi pamoja na wengine wakati wa chakula kilichoandaliwa kwa ajili yao na taasisi ya Al-Madinah Social Service Trust.
Karamu hiyo ilidhaminiwa na kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Meneja Rasilimali Watu wa IPTL, Aidan Kaude, aliyejumuika na watoto hao katika sherehe hizo, alisema kampuni yake imeona haja ya kuisaidia Al-Madinah katika kuhakikisha kuwa watoto hao wanapata haki ya kusherehekea wakati huu muhimu katika maisha ya waislamu wote duniani.
"Tulipopata maombi kutoka Al-Madinah kusaidia kufanikisha karamu hii, Mwenyekiti wetu Mtendaji Harbinder Sethi aliidhinisha haraka ombi hilo na kusema kuwa ni jambo la heri sababu watoto hao ni yatima na wanahitaji msaada kutoka kwa kila mtu waweze kuishi maisha ya kawaida kama wengine wanavyoishi licha ya kupoteza wazazi wao," alisema.
Mkurugenzi wa Al-Madinah Social Service Trust, Sheikh Ally Mubaraki, alisema kuwa baada ya kufanya kazi karibu na kwa muda mrefu na makundi mengi na taasisi mbali mbali za Kiislamu, taasisi yake imegundua kuwa yatima wengi wanakumbwa na changamoto nyingi ambazo ni pamoja na ukosefu wa mahitaji ya msingi kama vile chakula, mavazi na malazi.
Alisema taasisi yake iliomba msaada wa kifedha kutoka IPTL  kuwapatia msaada watoto waishio katika mazingira magumu nao wapate nafasi ya kusherehekea na Waislamu wenzao katika sikukuu hiyo.
Sherehe hizo zinahimiza Waislamu duniani kufanya yale yaliyoagizwa na Mtume Muhammad.

No comments: