WAKATA MAPANGA NG'OMBE NA KUCHOMA MTUMBWI WA WAVUVI

Wananchi katika Kijiji cha Mugara, Kata ya Iramba wilayani hapa wamewakatakata kwa mapanga ng’ombe wawili wa wavuvi waliodaiwa kufanya uvuvi haramu na kuteketeza kwa moto mtumbwi wao.
Imeelezwa kuwa wananchi hao walijichukulia sheria mkononi kwa kile walichodai kuwa, waliwakuta wavuvi hao wakitumia sumu kuvua samaki katika Ziwa Victoria. Pia waligawana nyama baada ya kuwachinja ng’ombe hao.
Mwenyeiti wa kijiji cha Mugara, Ngajeni Bituro pamoja na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Wilibard Marea walisema kwa nyakati tofauti kuwa, tukio hilo ni la juzi saa 8 mchana kijijini hapo.
 Walisema kuwa wavuvi hao Ngarya Musimu, jina maarufu ‘Kajee’, mkazi wa kijiji cha Nyakatuba na Kengera Gagi, mkazi wa kijiji Mugara, wilayani hapa, walikamatwa na wananchi hao wakivua kwa kutumia sumu na walishavua samaki zaidi 200 aina ya sato.
 Aidha, walisema kuwa kulingana na sheria ndogo walizojiwekea kijijini hapo, kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu mtu yeyote anayekamatwa akifanya kosa hilo, adhabu yake ni zana zake zote za uvuvi huo kuteketezwa kwa moto na kuchukuliwa ng’ombe wawili ama kulipa faini ya Sh 300,000.
Marea alisema wakazi hao baada ya kuwakamata wavuvi hao wenzao wawili walikimbia na kutokomea kusikojulikana.
Alisema kuwa wavuvi waliotoroka ni pamoja na Doi Wiliam Buriro na Kileo Kwibyira  ‘Rasi’, wote ni wakazi wa kijiji cha Kasahunga wilayani hapa.
Mtendaji huyo alisema wananchi wenye hasira walikwenda nyumbani kwa mtuhumiwa mmoja na kuwakatakata kwa mapanga ng’ombe wawili na kugawana nyama, ikiwa ni pamoja na kuuteketeza kwa moto mtumbwi mmoja uliohusika katika uvuvi huo.
Alisema kuwa wavuvi hao walikutwa wakivua samaki kwa sumu katika eneo la kisiwa cha Hilera katika Ziwa Vistoria na walipelekwa Kituo kidogo cha Polisi Kibara.
Viongozi hao wakiwemo wa Vikundi vya Ulinzi wa rasilimali za Ziwa Victoria (BMU) walisema kuwa wavuvi hao ni wazoefu kwenye uvuvi haramu.
 Hata hivyo walidai wavuvi haramu wamekuwa wakikamatwa na kuachiwa na vyombo vya dola, jambo linalowakatisha wananchi tamaa na kuamua kuchukua sheria mkononi wanapowakamata.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Philipo Kirangi, alisema jana kuwa bado hajapata taarifa kamili kuhusu tukio hilo, na kwamba atafuatilia na kulitolea ufafanuzi.

No comments: