WIZARA YASEMA TUHUMA ZA RUSHWA NI HISIA TU



Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema tuhuma za rushwa zinazoambatanishwa na kazi ya usaili wa nafasi ya Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji ni hisia tu za wahusika.
Taarifa  iliyotolewa na Msemaji wa wizara hiyo, Isaac Nantanga, inasema tuhuma za kuwapo kwa rushwa wakati wa kazi ya usaili ni hisia na hazina ushahidi na kuwa usaili ulifanywa kwa kufuata kanuni na sheria zinazosimamia ajira za watumishi wa umma.
“ Katika Uwanja wa Taifa ambao usaili ulikuwa ukifanyika kulikuwa na maofisa mbalimbali kutoka taasisi za wizara hiyo waliokuwa na kazi ya kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa usalama.”
Alisema, nafasi za Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji zilitangazwa katika magazeti na Tovuti ya Wizara na Idara ya Uhamiaji kufuatana na taratibu Serikali zinazosimamia ujazaji wa nafasi za kazi katika utumishi wa umma kwa lengo la kuiweka wazi kwa umma.
Nantanga alisema waombaji zaidi ya 20,000 walitumia haki yao ya msingi kuomba nafasi hizo na kutokana na wingi huo, Wizara ilifanya mchujo wa awali na kubakiwa na maombi 10,500 ya watu wenye sifa.
“Wizara ilitambua haki ya kila muombaji ya kupatiwa nafasi ya kushindania nafasi hizo, ikabidi ufanyike utaratibu wa kutafuta eneo lenye nafasi ya kutosha. 
“ Nia ya Wizara haikuwa kuleta usumbufu kwa mtu yeyote ila kutoa nafasi sawa kwa walioleta maombi kushindania nafasi zilizotangazwa,” alisema na kuongeza kuwa wingi wa watu ni matokeo ya kidemokrasia ya kutoa nafasi kwa kila raia kushindania nafasi za ajira zinazotolewa.
Akizungumzia baadhi ya changamoto walizozibaini, Natanga alisema ni kwa baadhi ya waombaji kufika katika eneo la usaili akiwa mikono mitupu bila kuwa na vifaa vya kawaida vya kushiriki usaili kama kalamu.

No comments: