HOSPITALI YA SINZA YAELEMEWA WAGONJWA



Hospitali ya Sinza   katika Manispaa ya Kinondoni inakabiliwa na msongamano mkubwa  unaodaiwa kuchangia  kuzorota utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
Diwani wa Kata ya Sinza, Renatus Pamba alitoa taarifa hiyo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani la manispaa hiyo. 
Kwa mujibu wa diwani huyo, hivi sasa hospitali hiyo inapokea watu kuanzia 1,500 kwa siku tofauti na awali ambapo idadi ya wagonjwa ilikuwa takribani 200. 
"Hivi sasa Hospitali ya Sinza imekuwa kama kimbilio la watu mbalimbali wanaohitaji matibabu hatua inayoifanya ielemewe tunaomba msaada wa dharura mahali pale ikiwemo ya kuongeza watoa huduma,"  alisema Pamba.
Aidha akipokea msaada wa vifaa mbalimbali vilivyokabidhiwa na uongozi wa Redio ya 'E fm' juzi, Mganga wa zamu wa hospitali hiyo,  Dk Ally Njama alikiri hospitali hiyo kulemewa wingi wa wagonjwa. 
"Tunawaomba watu wenye mapenzi mema kujitokeza kwa ajili ya kutupa misaada ili tuweze kuboresha huduma za hospitali yetu," alisema Dk Njama.
Alisema huduma zinazotolewa hapo ni kwa ajili ya wananchi mbalimbali hivyo ni muhimu kila mtu akajiona kuwa na jukumu la kujitoa katika suala zima la kutoa msaada.

No comments: