BARCLAYS YAZINDUA HUDUMA MPYA ZA KIBENKI



Benki ya Barclays nchini imezindua mfumo mpya wa utoaji huduma za kibenki nchini bila kutumia karatasi au kujaza fomu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana  jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kitengo cha Wateja Binafsi, Kumaran Pather alisema wanajivunia kuwa benki ya kwanza nchini kutumia mfumo wa utoaji wa huduma za kibenki kwa mfumo huo mpya.
Alisema kwamba mfumo huo wa kutoa huduma za benki bila kujaza fomu au karatasi ni moja tu ya huduma mbalimbali ambazo benki hiyo inaleta katika kuboresha huduma zake kwa wateja.
“Mfumo huu wa utoaji huduma za kibenki bila kutumia karatasi unachukua nafasi ya matumizi ya karatasi katika kupata huduma ikiwemo fomu mbalimbali za kutolea na kuchukulia pesa,” alisema.
Pather aliendelea kufafanua, “Uvumbuzi huu ni wa kisasa na tunajivunia kwa sababu wateja wetu sasa hivi wanatumia chini ya dakika tatu kuweza kukamilisha miamala yao ikiwemo kulipwa fedha taslimu, kuweka cheki, kutoa pesa na kubadili hundi kuwa pesa taslimu.” 
Aliongeza kuwa uvumbuzi huo umesaidia kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa katika kuhudumia wateja na pia unapunguza muda wa utoaji wa huduma kwa wateja.
Kwa upande wake, Meneja Miradi wa Barclays,  Jane Mbwilo alisema benki hiyo inakuwa ya kwanza kutumia mfumo huu nchini na kuwa benki ya kwanza kutumia mfumo wa kupitisha hundi  kwa mitambo inayojiendesha.
“Tumepiga hatua kubwa sana katika kuboresha huduma kwa wateja wetu na mfumo huu mpya wa kutoa huduma bila karatasi, wateja wetu wote wanaweza kutumia mfumo huu katika matawi yote ya Barclays nchini,” alisema. 
Aliongeza kuwa mkakati wa benki hiyo ni kutumia teknolojia ambayo itasaidia kurahisisha huduma kwa wateja pia na kupunguza gharama za uendeshaji wa benki.

No comments: