BODI YA MIKOPO YAKUSANYA SHILINGI BILIONI 49.7



Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imekusanya zaidi ya Sh bilioni 49.7 ya mikopo kutoka kwa wanufaika wa mikopo hiyo hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu.
Kiasi hicho cha fedha kilichokusanywa na Bodi ni sawa na asilimia 55 ya mikopo iliyopaswa kuwa imerejeshwa ya zaidi ya Sh bilioni 90.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Kaimu Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Asange Bangu wakati wa ufunguzi wa ofisi ya Bodi hiyo Kanda ya Ziwa.
Alisema hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu idadi ya wanufaika wa mikopo waliotafutwa na kujulikana  mahali walipo walikuwa 97,823 sawa na asilimia 68 ya wanufaika wote wa mikopo 143,281 ambao mikopo yao imeiva.
Bangu alisema idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu imezidi kuongezeka mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2005/06 wanafunzi walionufaika na mikopo walikuwa 42,729 waliokopeshwa kiasi cha Sh 56,111,371,485.
Alisema katika mwaka wa fedha 2013/2014, Bodi imekwishatoa mikopo kwa wanafunzi 95,241 ambao wamekopeshwa kiasi cha Sh 333,507,422,641, fedha ambazo zinajumuisha ruzuku kutoka serikalini na za urejeshwaji wa mikopo.
Alisema uanzishwaji wa ofisi za Kanda ni muendelezo wa utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Bodi uliolenga kusogeza huduma karibu na wadau wake na pia kuongeza kasi ya ukusanyaji wa marejesho ya mikopo iliyoiva.
Akizindua ofisi ya Bodi, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Baraka Konisaga alisema wastani wa wanafunzi wanaotakiwa kwenda elimu ya juu kwa Tanzania ni asilimia 3.9  wakati kwa nchi zilizo chini ya Jangwa la Saharani ni asilimia 5.
Konisaga alisema hali ya kuwa na kiwango cha chini kimechangiwa na ufinyu wa rasilimali fedha kwa wananchi jambo ambalo liliifanya Serikali kuanzisha utaratibu wa utoaji wa mikopo ili kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi kupata elimu.
 “Ili kujenga Mfuko endelevu utakaowawezesha wanafunzi wengi kunufaika, ni budi kuhakikisha mikopo inayotolewa inarejeshwa kwa wakati,” alisema Konisaga.
Alisema mara kadhaa limekuwa likizungumzwa suala la utoaji wa mikopo, lakini urejeshwaji wake haliguswi hivyo ni wajibu wa kila mzalendo aliyepata mkopo kuurejesha kwa ajili ya manufaa ya vizazi vijazo.

No comments: