NYALANDU AZINDUA KAMPENI KUPANDA MLIMA KILIMANJARO



Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu amezindua awamu ya 13 ya upandaji wa Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuchangia fedha za kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa ya Ukimwi.
Mpango huo uliopewa jina la Kili Challenge, unadhaminiwa na  Mgodi wa Dhahabu wa Geita kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) na watu 500 walipanda mlima huo. 
Akizungumza katika uzinduzi huo, Nyalandu alisema kuwa hatua ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuchangia fedha za kupambana na Ukimwi ni nzuri kwa kuwa inaongeza hamasa kwa wananchi katika kupambana na ugonjwa huo.
Alisema kuwa ni hatua ambayo wahusika wanaopanda mlima huo wanakuwa wametimiza dhana ya kutumia utalii katika kupambana na Ukimwi.
Nyalandu alisema pia unaongeza hamasa katika kusaidia Serikali kutimiza Malengo yake ya Milenia ya kuhakikisha kuwa hakuna maambukizi nchini hasa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
"Hii ni hatua nzuri kubwa na yenye tija kubwa kwa wanajamii kwa ujumla wake, kwa kuwa hawa wapandaji mlima wanakuwa wamechangia fedha zitakazosaidia mapambano dhidi ya Ukimwi kwa njia hii ambayo ni sehemu ya utalii,” alisema Nyalandu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS)  Fatma Mrisho alisema Watanzania kwa ujumla wanatakiwa kuungana na kila mmoja kwa wakati wake kupambana na ugonjwa huo.
Alisema kuwa changamoto kubwa kwa sasa ni katika kuhakikisha kuwa jamii inaondokana na hali ya unyanyapaa pamoja na kuondoa maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa watu milioni 1.6 wanaishi na virusi vya Ukimwi huku kukiwa na maambukizi mapya 86,000 kwa kila mwaka.
Akizungumza katika sherehe za uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Geita, Michael Van alisema kuwa mgodi huo utaendelea  kushirikiana na serikali katika kupambana na Ukimwi.

No comments: