IMANI YA FREEMASONS YALETA TAFRANI SINGIDA



Imani potofu ya kuunganishwa na dini inayodaiwa kuabudu shetani (Freemason) nusura ivuruge kazi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) ya kuandikisha majina ya kaya masikini, Wilaya ya Mkalama, mkoani Singida.
Imedaiwa kuna watu walisambaza ujumbe wa imani potofu kuwa watakaokubali kuorodheshwa majina yao wangeunganishwa na dini hiyo inayodaiwa kuwa inaabudu shetani.
Akizungumzia sakata hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwanga, Ezekiel Kamunga alisema alisikia suala hilo likizungumziwa juu juu na baadhi ya watu lakini hata hivyo hakuna ukweli wowote juu ya suala hilo.
Alisema ujumbe huo ulisambazwa na watu wenye nia ya kukwamisha kazi bila ya kuwa na sababu za msingi za kufanya hivyo.
"Haya maneno yapo ila sijahakikisha, baadhi ya watu wenye nia mbaya na chafu ya kufanya mpango huu usifanikiwe ndiyo wamesambaza hizi taarifa lakini hazina ukweli wowote," alisema.
Alisema katika kazi hiyo ililenga kuandikisha kaya 366 ambapo mpaka jana walikuwa wameshaandikisha zaidi ya kaya 150.
Kamunga alisema baada ya kukamilika kwa kazi hiyo kutasaidia kubaini ni kaya ngapi hazijaandikisha kutokana na vitisho hivyo na pia kumbaini aliyesambaza taarifa hizo.
"Sasa hivi bado tunaendelea na kazi ya kuwaandikisha, tukishamaliza ndiyo tutajua kaya ngapi hazijaandikishwa na kumtafuta mtu aliyesambaza taarifa hizi za uongo," alisema.
Kamunga aliwaomba wananchi kupuuzia kauli hizo alizoziita za mtaani kwani hazina ukweli na zinaenezwa ili kuvuruga mpango huo wenye nia ya kuwanufaisha wananchi.

No comments: