MABASI YA UDA KUWEKWA VIBAO VINAVYOONESHA NJIA



Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) limekubaliana na Mamlaka ya  Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra) kuweka vibao katika mabasi yake kuonesha njia yanakotoa huduma na si kupaka rangi.
Mkuu wa UDA, Hamdy Al Hadj alisema kibao kitakachowekwa, kitakuwa na rangi ya eneo husika kama ilivyo kwa daladala nyingine. 
“Kwa mfano kama basi linakwenda Gongo la Mboto basi katika kibao kilichoko mbele ya basi kiwe na rangi ya eneo hilo kama ilivyo katika daladala,” alisema Hamdy.
Alisema wanaendelea  kukamilisha uwekaji vibao hivyo pamoja na kuweka namba za wamiliki kwenye magari yote ili abiria waweze kutoa taarifa watakapohudumiwa tofauti. 
 “Tumeweka namba za simu nyuma ya mabasi ili kuwasaidia abiria kutoa taarifa pindi watakapokuwa wakipata huduma tofauti kwa mfano kupandishiwa nauli,” alisema na kuongeza kuwa namba hizo zimesaidia kupokea malalamiko mengi ya abiria kuhusu wafanyakazi wanaotoa huduma mbaya. 
Alihimiza abiria kusaidia kwa kutoa taarifa watakapohudumiwa isivyostahili ili madereva au makondakta watakaokiuka utaratibu wachukuliwe hatua.
Katika hatua nyingine, Kampuni  ya Simon Group Limited imesisitiza dhamira yake ya kuboresha Sekta ya Usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.  
“Tumeona taarifa ambazo zimekuwa zikichapishwa katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii …wakijaribu kuwafanya watu waamini kila uwekezaji unaofanywa katika kuboresha mfumo wa usafiri jijini Dar es Salaam kupitia UDA hauna maana,”  alisema Ofisa Mtendaji Mkuu, Robert Kisena kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.
Alisema mpango ambao kampuni imedhamiria kuboresha huduma ya usafiri Dar es Salaam, uko pale pale ukihusisha mradi wa kuwa na mabasi zaidi ya 3,000 pamoja na mabasi mengine ya kifahari 50 yenye viyoyozi na huduma ya intaneti.
Alisema kwamba tathmini inaonesha kuwa ili kuwezesha mabasi yapatayo 3,000 kufanya kazi hapo baadaye wataalamu wapatao 7,800 watahitaji kupewa mafunzo na kuajiriwa.
Aliongeza kwamba mara baada ya mpango huo kukamilika, unyanyapaa miongoni mwa wanajamii kuhusu utumiaji wa mabasi ya uma hautokuwepo tena na watu wataacha kupaki magari yao katikati ya Jiji, watanunua tiketi za UDA kwa njia ya mtandao.
“Ninataka kuwahakikishia Watanzania wote na wale wanaoendelea na kampeni zao kwamba mpango wa UDA kuboresha mfumo wa usafiri Dar es Salaam ni jambo linalowezekana, Tutafanya kazi kwa karibu na Serikali pamoja na Jiji ili kuona wakazi wa Dar es Salaam wanapata huduma rahisi na ya uhakika ya usafiri,’’ alisema Kisena.

No comments: