UCHAGUZI MKUU CUF KUFANYIKA WIKI IJAYO



Safu mpya ya uongozi wa Taifa ya Chama cha Wananchi (CUF) inatarajiwa kupatikana mwezi huu katika uchaguzi utakaofanyika wiki ijayo, jijini Dar es Salaam. 
Chama hicho kinachoongozwa na Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba, Makamu wake,  Machano Khamis Ali  na Katibu Mkuu, Seif Sharif Hamad, kitafanya mkutano wake mkuu Juni 23 hadi 27 utakaokwenda sanjari na uchaguzi wa viongozi.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu, Hamad alisema maandalizi yote ya msingi kwa ajili ya mkutano huo yamekamilika. 
Alisema watawachagua viongozi wakuu wa kitaifa wa chama hicho ambao ni Mwenyekiti wa Taifa, Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu.
Viongozi wengine watakaochaguliwa katika mkutano huo ni wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa pamoja na wajumbe wa Viti Maalumu vya Wanawake.
Alisema katika mkutano huo, wajumbe watapokea taarifa mbalimbali za kazi za chama kuanzia mwaka 2009 hadi 2014 ambapo pia watapata fursa ya kuzijadili.
Kwa mujibu wa Hamad, chama kinaendelea na vikao mbalimbali kikiwemo cha Kamati ya Utendaji, ikiwa ni maandalizi ya mwisho kwa ajili ya mkutano huo kabla ya wajumbe kuwasili kwa ajili ya mkutano huo wa kitaifa.

No comments: