WIKI YA MAJIBU YA WAZIRI WA FEDHA YAANZA



Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, anasubiriwa wiki hii kutegua kitendawili cha hoja za wabunge, kuhusu punguzo la kodi katika mishahara,  vyanzo vipya vya mapato na utekelezaji wa miradi wa maendeleo.
Leo ndio siku ya mwisho kwa wabunge kujadili hotuba ya bajeti ya Waziri Saada  na kesho Waziri ataanza kujibu hoja akishirikiana  na Naibu wake, Mwigulu Nchemba na Adam Malima.
Katika majibu yake, Waziri Saada anatarajiwa kuonesha namna Serikali ilivyojipanga kusimamia nidhamu ya makusanyo na matumizi ya fedha za Serikali, ikiwemo hatua aliyoitangaza ya kufuta misamaha ya kodi isiyo na tija.
Wabunge wengi, pamoja na kuipa Serikali changamoto, walielezea kuridhika na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika majimbo yao, hasa miradi ya umeme vijijini na maji.
Pia ufikishaji wa bomba la gesi Dar es Salaam ni moja ya miradi inayoipa Serikali sifa kwa kuwa matarajio ni Serikali kuacha kutumia fedha nyingi katika ununuzi wa mafuta ya dizeli na petroli kwa ajili ya uzalishaji umeme.
Aidha, bei ya nishati hiyo kutoka kwa kampuni zinazofua umeme, inatarajiwa kushuka kutoka senti za Marekani 30 na 60 kwa uniti moja mpaka chini ya senti 18 za Marekani kwa uniti moja na kusaidia Serikali kutekeleza nia yake ya kushusha bei ya umeme.
Nafuu hiyo ya bei ya umeme, mbali na kuleta nafuu ya maisha kwa mwananchi mmoja mmoja mijini mpaka vijijini, inatafsiriwa kuwa kivutio cha uwekezaji, kitakachochangia ongezeko la ajira na ukuaji wa uchumi wa nchi  ambao kwa sasa ni asilimia  saba.
Katika mijadala ya wabunge, wengi walipongeza hotuba ya Bajeti na kutaka maoni ya Kamati ya Bajeti, inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), yazingatiwe  kuboresha upatikanaji wa mapato.
Katika maoni ya Kamati hiyo, Chenge alisema  upo udhaifu wa Serikali katika utekelezaji wa bajeti, kutokana na kuendelea kutegemea vyanzo vile vile vya mapato, huku matumizi yake yakiwa makubwa ikilinganishwa na mapato.
Akiwasilisha taarifa yake, Chenge alisema kamati yake imeshitushwa na ukuaji wa deni la taifa, akisema ilo ni mzigo mkubwa. Alisema hivi sasa deni hilo ni tishio kwa uchumi wa taifa. 
“Serikali imeendelea kuja na vyanzo vile vile vya kiutamaduni vilivyozoeleka, ambavyo ni pombe, sigara, vinywaji baridi na vinywaji vikali, wakati kuna vyanzo vingine vingi,” alisema Chenge. 
Alitaja baadhi ya vyanzo vipya ambavyo Kamati yake inaamini vinaweza kuingizia Serikali mapato mengi, ni pamoja na uvuvi wa Bahari Kuu, kupiga mnada vitalu vya misitu na uwindaji wa kitalii, kupiga mnada masafa ya mawasiliano pamoja na kodi za majengo. 
Kwa mujibu wa Chenge, Kamati yake inashangazwa na majibu yanayotolewa na Serikali kuhusu suala la ukusanyaji wa mapato katika uvuvi wa Bahari
Kuu, kwamba haiwezi kukusanya hadi itakapojenga bandari maalumu ya uvuvi.
 “Kwa taarifa rasmi za Serikali zilizotolewa bungeni, Serikali inapoteza takriban Dola za Marekani milioni 222, sawa na Sh bilioni 372.9. Kamati inahoji hadi hapo tutakapojenga bandari maalumu ya uvuvi, tutakuwa tumepoteza mapato kiasi gani,” alihoji.
Alisema Kamati yake imechambua bajeti ya mwaka 2013/2014 na kubaini kuwapo kwa madeni makubwa katika baadhi ya wizara na taasisi mbalimbali za umma.
“Mfano Wizara ya Ujenzi imekuwa ikitekeleza miradi ya ujenzi wa barabara bila kuwalipa makandarasi kwa wakati na kwa kuzingatia mikataba yao na hivyo kujikuta ikianza kila mwaka wa fedha ikiwa na malimbikizo makubwa ya madeni.
 “Hali hii imesababisha Wizara hii kutumia bajeti yake ya mwaka unaofuata kulipia madeni ya mwaka uliopita, badala ya kutekeleza miradi iliyoidhinishwa kwa mwaka husika wa fedha,” alisema Chenge.
Akizungumza kuhusu deni la taifa, Chenge alisema licha ya Serikali kusema deni hilo ni himilivu, lakini kwa uhalisia deni hilo ni mzigo mkubwa kwa taifa linaloathiri uchumi wa nchi.
“Hadi kufikia Machi 2014, deni la taifa linalojumuisha deni la Serikali na deni la nje la sekta binafsi lilifikia Sh trilioni 30, ikilinganishwa na Sh trilioni 23 mwezi Machi, 2013,” alisema.
Chenge alitoa sababu kadhaa zinazoifanya Kamati yake ishindwe kukubaliana na hoja ya Serikali kwamba deni hilo ni himilivu.
“Mosi, kuna madai mengi ya ndani ambayo hayajajumuishwa katika deni la taifa na taarifa zilizopo zinaonesha kuwa madai haya yanaendelea kuongezeka.
Sababu nyingine ni kwamba,  uwiano uliopo wa deni la taifa na pato la Taifa kiuchumi si wa kuridhisha, ukubwa wa deni hili hauwiani na kiwango cha uzalishaji na ukuaji wa uchumi wa sasa wa asilimia saba.
 Pia alisema, udhaifu katika usimamizi wa matumizi ya fedha za umma na ucheleweshaji wa uhakiki wa madai ya ndani ni sababu nyingine. Taarifa ya Waziri wa Fedha ya nusu mwaka inaonesha, malimbikizo ya madai hadi Desemba, 2013 yalikuwa yamefikia Sh trilioni 2.09, ambayo ni asilimia  nne ya pato la Taifa,” alisema.
Wabunge wengi pia walisema punguzo la Kodi katika Mshahara (Paye), kutoka asilimia 13 mwaka unaoisha wa fedha 2013/2014 mpaka asilimia 12 kwa mwaka ujao wa fedha 2014/2015, kuwa ni ndogo.

No comments: