BODABODA ZAUA WATU 218, KUJERUHI 1,304 TANGU JANUARI



Polisi imetangaza operesheni nchi nzima ya kukamata madereva wa pikipiki (bodaboda), wasiofuata sheria za usalama barabarani, wakiwemo wanaopita  taa nyekundu bila kuruhusiwa.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alitoa tamko  jijini Dar es  Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Licha ya operesheni kulenga kudhibiti madereva wa vyombo hivyo wanaopita taa nyekundu, makosa mengine yatakayosababisha sheria kuchukua mkondo wake ni kutozingatia alama na michoro ya usalama barabarani.
Operesheni hiyo itagusa waendesha pikipiki za kawaida, za miguu mitatu(bajaj), baiskeli na maguta, ambazo kwa mujibu wa Polisi, zimekuwa zikikiuka utaratibu na sheria za usalama barabarani.
“Jeshi la Polisi limekuwa likifanya juhudi za kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua, lakini bado kuna baadhi ya waendesha pikipiki, baiskeli na maguta wamekuwa vinara wa kukiuka sheria, utaratibu na kanuni za usalama barabarani.”
“Ukiukwaji huo unachangia ongezeko la ajali za mara kwa mara ambazo zinaweza kuzuilika, hivyo tunaanzisha operesheni ya kubaini, kukamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria na kuwafikisha mahakamani.”
Kwa mujibu wa Senso, kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, ajali 1,449 zilizosababishwa na bodaboda zilitokea na kusababisha vifo 218 na majeruhi 1,304.
Alipoulizwa na waandishi wa habari  juu ya kuwapo tabia ya baadhi ya polisi kutumia operesheni kama hizo, kujiingizia kipato binafsi kwa kupokea rushwa, Senso alisema, Polisi haijaanzisha operesheni hiyo kwa lengo hilo.
“Operesheni hii ni  kwa ajili ya kuhakikisha madereva wanafuata sheria za usalama barabarani,” alisisitiza Senso.
Ingawa  Senso alisisitiza operesheni hiyo kulenga madereva wanaokiuka sheria, kumekuwepo na malalamiko dhidi ya baadhi ya askari, kugeuza madereva hao kama mradi wa kujiingizia vipato binafsi.
Licha ya malalamiko kujitokeza kutoka maeneo mbalimbali nchini, kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam, baadhi ya askari waliobatizwa jina la ‘Tigo’ pamoja na baadhi ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, wanadaiwa kutoza faini za papo kwa hapo bila kutoa risiti.
Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam walipendekeza Jeshi hilo la Polisi, hasa trafiki, waanze kuanzia sasa kutumia Mashine za Kielektroniki za Malipo  (EFDs) za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kutoza faini za makosa ya usalama barabarani.
Walisema utaratibu wa sasa wa trafiki, kutumia lundo la vitabu barabarani,  linatia hofu kuwa fedha nyingi wanazotozwa madereva wa magari au bodaboda kama faini, hazifikishwi serikalini, kwani kama zingefikishwa Serikali ingekuwa na fedha nyingi.
 Walisema mashine hizo za TRA, ndizo pekee zitakazodhibiti fedha za Serikali na kuziba mianya yote ya ulaji wa trafiki.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo la Polisi limetaka vikundi vya ngoma kufuata taratibu kwa kuwa na vibali kutoka halmashauri za maeneo husika ili kuzuia mianya ya ukiukaji maadili na kutoa mianya ya uhalifu.
“Polisi inakemea tabia iliyoibuka ya vikundi vya ngoma maarufu kama vigodoro vinavyojihusisha na kupiga muziki au ngoma mitaani na kufunga barabara kinyume na taratibu,” alisema.

No comments: