UVCCM YAPINGA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR

Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) imesema kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar si tiketi itakayoweza kumsaidia Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad kushinda na kuwa Rais wa Zanzibar katika  uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.
Naibu Katibu Mkuu wa  UVCCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka alisema hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Binti Amran Jimbo la Mpendae, Kisiwani Unguja .
Shaka alisema si jambo  rahisi kama inavyofikiriwa na baadhi ya viongozi wa CUF kudai   Maalim Seif  mwaka 2015  atashinda kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya sasa, Maalim Seif ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Katika mkutano huo, Shaka alizungumzia pia masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuitaka Serikali kuwakabili na kuwaasa viongozi wanaochanganya dini na siasa ili  kwa kutumia nafasi zao wasiweze kuleta madhara kwa jamii.
Akizungumzia  matukio ya uhalifu katika ukanda wa Afrika Mashariki sambamba na milipuko ya mabomu katika miji ya Mombasa, Arusha na Zanzibar, Shaka alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano  ili kukabiliana na tishio hilo.
Aliviomba vikosi vya ulinzi na usalama kuwa makini katika kipindi hiki kigumu kuliko wakati wowote,  kufanya kazi kwa pamoja ili kubaini mitandao ya kihalifu akisema ikiwa mazingira ya utulivu na amani yatatoweka, hakutakuwa na mipango ya maendeleo aidha ya kiuchumi, kisiasa au kijamii.

No comments: