MATUMIZI YA NISHATI YA MAGOGO YAKERA WADAU

Wakati Serikali ya Tanzania ikiungana na nchi za Kenya na Uganda na Umoja wa Mataifa kupiga vita biashara ya magogo katika nchi za ukanda wa maziwa makuu, uongozi wa kiwanda cha kutengeneza nguo cha Sunflag cha jijini hapa umeendelea kutumia magogo kuendeshea mitambo ya kiwanda hicho kikongwe nchini.
Katika azimio lililopitishwa Alhamisi wiki hii jijini Nairobi nchini Kenya na  Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA), nchi za Tanzania, Kenya na Uganda zilikubaliana kwa pamoja kuungana na umoja wa Mataifa kupinga uvunwaji wa magogo katika nchi hizo ili kunusuru uharibifu mkubwa wa mazingira ambao unaelezwa kufanyika katika ukanda wa maziwa makuu.
Kwa mujibu wa Msemaji wa kiwanda cha Sunflag, Harun Mahundi, kiwanda hicho kimekuwa kikitumia magogo kwa miaka kadhaa sasa baada ya kuacha kutumia mafuta mazito kutokana na upatikanaji wake na gharama zake kuwa kubwa.
Meneja wa shamba la miti la Serikali la Olmotony lililoko Arumeru, jijini Arusha, Khadija Kiimu alipoulizwa kuhusu uuzaji wa magogo hayo licha ya kupigwa marufuku, alikiri ofisi yake kuuza magogo yanayotokana na miti inayozalishwa katika msitu wake kwa wafanyabiashara mbalimbali ijapokuwa hakuwa na uhakika wa mahali ambapo magogo hayo yamekuwa yakipelekwa.

No comments: