DC AMWAGA CHOZI KWENYE MKUTANO WA HADHARA

Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu, juzi aliwashangaza wengi baada ya kuangusha machozi mbele ya wananchi waliofurika kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Mtunguru, Kata ya Bukoko wilayani hapa.
Kingu alianza kutokwa na machozi hata kabla ya mkutano, baada ya kuoneshwa na Mwenyekiti wa kijiji hicho, Siminzaga Mange nyumba ya mwalimu iliyojengwa kwa nguvu za wananchi zaidi ya miaka minane lakini mpaka sasa haijamaliziwa kwa kupauliwa.
Nje na nyumba ya mwalimu, Kingu aliendelea kutokwa na machozi alipoambiwa kuna jengo la nyumba ya mganga ambalo nalo limejengwa kwa nguvu za wananchi lakini bado halijapauliwa mabati na serikali licha ya wananchi kuchangia nguvu zao.
Mkuu huyo, baada ya kutembea katika kijiji hicho kwa miguu kwa zaidi ya kilomita 30 akijionea miradi mbalimbali ya maendeleo, alikaribishwa na Mwenyekiti wa kijiji azungumze na wananchi ili awahamasishe kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Akizungumza, huku akiendelea kutokwa na machozi, alisema: “Ndugu zangu wananchi wa kijiji cha Mtunguru mimi nimesikiliza maelezo ya mwenyekiti wenu wa kijiji na kujionea mengi, nimeumizwa sana…haiwezekani wananchi wanachangia nguvu zao halafu sisi kama serikali tunashindwa kukamilisha majengo hayo hii ni aibu kubwa kwa serikali.
“Kwa kuanzia, mbao zote 670 zilizokamatwa na maliasili zitatumika kupaua nyumba ya mwalimu pamoja na nyumba ya mganga na mtu yeyote atakayehoji mimi nitajibu kwa niaba ya serikali.
“Mabati na saruji nitatoa mimi mwenyewe, hivyo lazima watendaji wa vijiji na vitongoji msimamie kwa makini mbao hizo, mabati na saruji nitakavyovileta. Atakayeonekana kukwapua vitu hivi nawaambieni sitasita kumkamata na kumpeleka katika vyombo vya sheria.”
Kutokana na kauli hiyo, wananchi walishangilia na wamempongeza mkuu huyo kwa uamuzi aliouchukua.

No comments: