TPSF YAHIMIZA MAADILI KWENYE BIASHARA

Wafanyabiashara wametakiwa kufuata maadili ya biashara ili kuepusha rushwa katika biashara.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Taasisi ya sekta binafsi(TPSF), Gideon Kaunda (pichani kushoto) katika mkutano na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP) katika uzinduzi wa kanuni za utawala bora katika biashara.
Alisema suala la rushwa halipo upande mmoja ni muhimu kuhakikisha wafanyabiashara wanaepuka rushwa kwani wafanyabiashara wote sio safi hivyo ni lazima hatua zichukuliwe kwa wafanyabiashara wote.
Alisema kanuni hizo zitasaidia kuleta maendeleo ya uchumi kwani  UNDP wataleta misaada ambayo itasaidia kueneza utawala bora na kuhamasisha watu katika mikoa yote kuepuka rushwa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Daniel Machemba alisema uzinduzi huo ni juhudi za umoja wa mataifa kwa wafanyabiashara katika kuondoa rushwa kwenye biashara.
“Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakipenda utajiri wa haraka na kuleta biashara ambazo hazina ubora ili wao wafanikiwe kwa haraka,” alisema Machemba.
Naye Mshauri mwandamizi wa Utawala, Steve Lee alisema uzinduzi huo ni muhimu kwani utawasaidia wafanyabiashara  kuelewa maadili na kuepukana na masuala yote ambayo yanaweza kusababisha rushwa katika biashara.

No comments: