MBUNGE ALIA NA MRADI WA UMEME WA UPEPO SINGIDA

Mbunge wa Viti Maalumu, Christina Mughwai ameitaka serikali ieleze kwa nini inachelewa kutekeleza  Mradi wa Umeme wa Upepo Singida.
“Katika jitihada za kutatua tatizo la umeme nchini, serikali ilianzisha Mradi wa Umeme wa Upepo Singida kwa ushirikiano na NDC na Tanesco. Je, utekelezaji wa mradi huo umefika wapi ; na Je, ni lini mradi huo utakamilika?” aliuliza Mughwai ambaye ni mbunge wa Chadema.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga alisema serikali haijachelewesha mradi huo.  
Alifafanua kuwa mradi huo umeshafanyiwa  maandalizi ya kutosha, ikiwa ni pamoja na upembuzi yakinifu, uhakiki wa ufadhili na uwezo wa ujenzi wa mitambo.
Alisema serikali kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) imeshughulikia vibali vyote vinavyohitajika ili mradi utekelezwe, ikiwa ni pamoja na hatimiliki ya eneo la mradi, mkataba wa ununuzi wa umeme, cheti cha mazingira na hati ya vivutio vya uwekezaji. Alisema NDC ikishirikiana na Wizara ya Fedha, inafanya utaratibu wa kupata mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya China.
Kitwanga alisema gharama za uwekezaji katika awamu ya kwanza ya mradi huo na ujenzi wa miundombinu, zitakuwa ni dola za Marekani milioni 136.
Katika awamu ya kwanza, mradi huo unatarajiwa kuanza kufua umeme wa megawati 50 na baadaye utapanuliwa hadi kufikia megawati 300. Umeme utakaofuliwa utaunganishwa katika Gridi ya Taifa kupitia kituo kikuu cha umeme mjini Singida.
Kitwanga alisema mradi huo wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za upepo mkoani Singida, unatakelezwa na kampuni ya Geo Wind Power Tanzankia Limited, ambayo ni ubia kati ya NDC, Shirika la Umeme nchini (Tanesco) na kampuni ya Power Pool East Africa Ltd (PPEAL). NDC ina hisa asilimia 60, Tanseco asilimia 20 na PPEAL asilimia 20. Mradi huo upo katika vijiji vya Mughamo, Unyankanya na Kisasida.

No comments: