MAKAMPUNI 400 KUSHIRIKI MAONESHO YA 38 YA BIASHARA

Jumla ya kampuni 400 za nje zinatarajiwa kushiriki katika Maonesho ya 38 ya biashara ya kimataifa yanayotarajiwa kuanza Juni 28 mwaka huu katika viwanja vya maonesho vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam zikiwemo 11 za Kimarekani na tatu za Jamhuri ya wa Czech kwa mara ya kwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Jacqueline Maleko alisema mpaka jana tayari kampuni 1,260 za kitanzania zilithibitisha kushiriki na kuwataka washiriki wamalize ujenzi wa mabanda yao mpaka kufikia Juni 26.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa hii ni mara ya kwanza kwa washiriki kutoka mataifa ya Marekani na Jamhuri ya Czech kushiriki maonesho hayo, hivyo kuwataka wajasiriamali wa kitanzania kutumia fursa hiyo kujifunza na kupata uzoefu kutoka kwao kwani lengo la maonesho hayo ni kutengeneza ajira na si kuuza bidhaa.
“Hii ni mara ya kwanza kwa kampuni za kimarekani na Jamhuri ya Watu wa Czech kuja kushiriki maonesho haya. Hivyo tunataka maonesho yakiisha tuone fursa kwa wajasiriamali wetu kujitengenezea ajira kutokana na ujuzi na uzoefu watakaoupata kutoka kwa wenzao,” alisema.
Akizungumzia maonesho hayo, Mkurugenzi huyo alisema maonesho ya mwaka huu yatakuwa na msisimko zaidi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya washiriki toka mataifa mbalimbali ya nje jambo lililowalazimu kuongeza eneo katika viwanja hivyo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara za Nje wa Mamlaka hiyo, Anna Mulondo alisema utaratibu wa uingiaji katika viwanja hivyo pamoja na nauli haujabadilika na kubaki kama mwaka jana kwa lengo la kuongeza hamasa kwa wananchi na watu kutoka nchi nyingine kwenda kwa wingi kutazama maonesho hayo.
Alisema kwa upande wa nauli, mtu mzima atalipa Sh 2,500 huku mtoto akilipa Sh 500 kwa siku zote za maonesho isipokuwa siku ya kilele cha maadhimisho hayo ambayo ni Julai 7 kiingilio kwa mtu mzima kitakuwa ni Sh 3,000 wakati mtoto atalipia Sh 1,000.
“Utaratibu wetu ni ule ule wa mwaka jana haujabadilika. Magari hayataruhusiwa kuingia ndani, kuna maeneo maalumu ya maegesho nje ya viwanja na hivyo tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kuja kutazama maonesho hayo,” alisema.
Maonesho hayo ya Biashara ya Kimataifa ya 38 yanatarajiwa kuanza juni 28 na kumalizika Julai 8 mwaka huu katika Viwanja vya Maonesho vya Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.

No comments: