Serikali
imesema kuwa Mpango wa Pensheni kwa Wazee nchini, haujaanza kutekelezwa
kutokana na kutokamilika kwa maandalizi.
Naibu
Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga alisema hayo bungeni mjini hapa
jana, alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Leticia Nyerere (Chadema).
Dk
Mahanga alisema kuwa hadi sasa kazi zifuatazo zimekamilika: Rasimu ya awali ya
Mpango wa Pensheni kwa Wazee imeandaliwa; na ziara za mafunzo zimefanyika
katika nchi za Kenya, Uganda, Mauritius, India, Thailand, Singapore, China na
Indonesia.
Lengo
la ziara hizo zilizohusisha pia wabunge, lilikuwa ni kujifunza na kupata uzoefu
wa nchi nyingine katika kuendesha mipango ya pensheni kwa wazee.
Alisema
maeneo ambayo maandalizi hayajakamilika ni pamoja na kubaini vyanzo endelevu
vya mapato, vitakavyotumika kugharimia mpango huo, kuunda chombo
kitakachosimamia pensheni, kupata maoni kuhusu mpango unaopendekezwa kutoka kwa
wadau na taasisi zinazohusika; na kuwasilisha mpango huoĆ katika vyombo vya
maamuzi.
Katika
swali lake, Leticia alihoji "Tarehe 10 Oktoba 2010, Mheshimiwa Waziri Mkuu
katika Siku ya Wazee Duniani aliahidi wazee kupewa mafao yao. Je, ni kwa nini
mpango huo haujatekelezwa mpaka sasa?"
Akifafanua,
Naibu Waziri alisema serikali inatambua umuhimu wa kuhakikisha watu wake wote,
ikiwa ni pamoja na wazee, wanapata kinga ya hifadhi ya jamii.
Alisema
katika kutekeleza azma hiyo , mwaka 2003 serikali ilipitisha Sera ya Taifa ya
Hifadhi ya Jamii. Pamoja na mambo mengine sera hiyo, inaelekeza kuanzishwa kwa
programu za misaada ya jamii, inayojumuisha pensheni ya jamii kwa wazee
(universal pension).
Dk
Mahanga alisema tamko la Waziri Mkuu la Oktoba Mosi 2010 wakati wa kuadhimisha
Siku ya Wazee Duniani, lilitoa mwongozo wa kushughulikia suala la pensheni kwa
wazee kwa kuagiza mamlaka zinazohusika, kuchukua hatua stahiki. Baada ya hapo,
Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), ambayo
ndiyo kwanza ilikuwa imeanzishwa, ilipewa jukumu la kushughulikia suala hilo.
No comments:
Post a Comment