GHASIA AZUNGUMZIA MAANA PANA YA MIPANGO MIJI



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia amesema mipango miji si kupima viwanja pekee kama inavyofanywa sasa bali ni kuzingatia mahitaji mengine ya jamii kwa ajili ya maendeleo.
Ghasia alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam kwenye kongamano kuhusu uendelezaji wa mipango miji na majiji kwa maendeleo endelevu lilioandaliwa na taasisi ya Uongozi Institute.
Alisema halmashauri nyingine zimekuwa na dhana ya kupanga miji wa kuangalia upimaji wa viwanja vya makazi pekee na kusahau huduma nyingine zilizomuhimu kwa jamii.
'Mipango miji si kupima viwanja vya makazi peke, ni lazima kuzingatia maeneo ya viwanda, burudani na hata sehemu ya kupumzishwa pindi maisha yetu hapa duniani yanafikia mwisho,' alisema.
'Kwa sasa upangaji miji unaendana kivyake na mipango ya maendeleo inaenda kivyake. Tutafakari jinsi ya kupanga miji yetu vizuri,' alisema.
Ghasia alisema miji na majiji iliyopangwa vizuri ina uwezo wa kutoa huduma nzuri kwa wananchi.
Aidha, Ghasia alipongeza hatua ya kuwashirikisha mameya wa miji na majiji badala ya hali ya sasa ya kushirikisha wataalamu na wakurugenzi pekee ambao wamekuwa wakihama kila siku.
"Pamoja na meya ni mwanasisasa lakini ni mwananchi wa eneo hilo, hivyo kama hatakuwa madarakani atakuwa mwananchi ambaye kama atashirikishwa, basi ni rahisi kufahamu mipango ya miji iliyopo," alisema.
Ghasia aliwataka aliwataka washiriki wa kongamano hilo kutoka halmashauri na manispaa za miji na majiji, wataalamu wa mipango miji wahandishi wa izara pamoja na watafiti kutoka ndani na nje ya nchi kutoa mawazo chanya ili kuboresha hali ya miji na majiji nchini.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja alisema sekta ya ardhi haijatazamwa vizuri na kushauri kubadilishwa kwa sheria za upangaji mijikuanzia ngazi ya taifa hadi ile ya nchi.

No comments: