SERENGETI YAPOTEZA ZAIDI YA TEMBO 87 KWA MIAKA MITANO


Wakati Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na wadau wa uhifadhi wakitafuta mbinu za kuzuia mauaji ya tembo yanayoendelea kwenye hifadhi mbalimbali nchini, zaidi ya tembo 87 wameuawa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mhifadhi Utalii katika hifadhi hiyo, Godson Kimaro alisema hayo wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kutoka Chama cha waandishi wa habari mkoa Kigoma wanaofanya ziara za mafunzo katika hifadhi mbalimbali nchini.
Kimaro alisema katika idadi hiyo ya tembo waliouawa ipo idadi ndogo ya tembo ambao walikufa kwa magonjwa na uzee huku idadi kubwa wakiuawa na majangili na kung’olewa meno yao.
Aidha Mhifadhi huyo alisema kuwa katika kipindi hicho pia wanyama aina ya nyumbu 8,766 waliuawa na majangili kukiwa na idadi ya wanyama 17,252 ambao waliuawa na majangili kwa ajili ya kupata kitoweo na vitu mbalimbali walivyonavyo wanyama hao.
Akitoa takwimu kuhusiana na suala hilo la ujangili, Mhifadhi huyo wa hifadhi ya taifa ya Serengeti alisema kuwa jumla ya majangili 4,733 walikamatwa ambapo kesi 1,589 zilifunguliwa na kesi 1,822 zilikuwa zikiendelea katika hatua mbalimbali  na kiasi cha Sh bilioni 1.9 kilikusanywa ikiwa ni faini kutokana na hukumu zilizotolewa mahakamani.
Katika hatua nyingine Kimaro alisema jumla ya ekari 728 za mazao mbalimbali ya wananchi wanaoishi kuzunguka hifadhi ya Serengeti ziliharibiwa na wanyama katika matukio 214 ambayo yalihusisha tembo 779.
Akitoa maelezo, Mhifadhi Seth Mihayo kutoka idara ya utalii alisema kwa sasa hifadhi ya Taifa ya Serengeti inakadiriwa kutembelewa na watalii 400,000 kila mwaka ambapo kati yao Watanzania wakiwa watalii wa ndani ni asilimia saba ya idadi hiyo.
Akizungumzia suala la ujangili nchini, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa nchini (Tanapa),Witness Shoo alisema shirika hilo kwa kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali wako kwenye mpango mkakati wa kupambana na vitendo vya ujangili hasa mauji ya tembo ambao wako kwenye hatari ya kutoweka.
Hivi karibuni Wizara ya maliasili na utalii ilipewa Helikopta moja na mdau wa uhifadhi kutoka Marekani kwa ajili ya kusaidia shughuli za uhifadhi ikiwemo kupambana na vitendo vya ujangili wa kuuawa kwa tembo.

No comments: