SERIKALI YAPIGA MARUFUKU TRAFIKI KUVIZIA MAGARI

Serikali imepiga marufuku tabia ya askari Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, kuvizia magari katika barabara kuu wakiwa na kifaa cha kupima mwendo kasi wa magari.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Peraira Silima, alisema tabia hiyo ya trafiki ni kinyume cha sheria na zinaweza kusababisha ajali.
 Hata hivyo, Silima aliwataka madereva kutii Sheria za Barabarani ikiwemo kupunguza mwendokasi na kufafanua kuwa, wakati mwingine askari hutafuta kivuli na hatua hiyo isichukuliwe kuwa wanavizia magari.
Katika swali lake, Ngoye alitaka Serikali ieleze ni hatua gani zimekuwa zikichukuliwa kuhakikisha madereva wanafuata sheria zilizowekwa kama inavyofanyika katika nchi nyingine.
Ngoye pia alitaka Serikali ieleze kwa nini madereva wameendelea kutumia magogo, mawe na majani yenye miba barabarani kuashiria kuwa kuna gari limeharibika, na wakiondoka wanayaacha na wengine wameendelea kuendesha magari huku wakisikiliza simu.
 Naye Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (Chadema), alihoji kama ni sahihi kwa trafiki kuvizia magari na kifaa cha kupima mwendo kasi.
 Akifafanua majibu ya maswali hayo, Silima alisema trafiki kujificha na chombo hicho na kujitokeza kumilika gari ni kinyume cha sheria  kwa kuwa tabia hiyo inaweza kusababisha ajali.
 Kuhusu matumizi ya magogo, majani na mawe, alisema ni kinyume na Sheria na kutaka madereva watumie alama za pembe tatu ambazo ni nzito na kuachana na alama hizo ambazo ni nyepesi ambazo hupeperushwa na upepo.
 Silima pia alionya kuwa Serikali iko mbioni kuanza kuwanyang’anya leseni za udereva madereva wote ambao watathibitika kukithiri kwa makosa ya usalama barabarani, na kuzuiwa kabisa kufanya kazi hiyo.
 Hatua hiyo itaanza kuchukuliwa mara baada ya kukamilika na kuanza kwa Mfumo mpya wa Nukta, ambao utaweka kumbukumbu za makosa ya madereva ambayo itatumika kuwachukulia hatua hiyo.

No comments: