MWAROBAINI WA MSONGAMANO WA MAGARI WAPATIKANA



Utaratibu mpya wa kudhibiti msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, umetangazwa ambao utekelezaji wake utakapoanza, pikipiki na bajaj hazitaruhusiwa kuegeshwa wala kuendeshwa katika njia za waenda kwa miguu. 
Utekelezaji huo unaotarajiwa kuanza hivi karibuni, umelenga  kuondoa msongamano, kuimarisha usalama na usafi katika njia zote zilizokamilika za Mradi wa Mabasi  yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart). 
Awamu ya kwanza ya mradi, inatekelezwa kutoka Kimara hadi Kivukoni; Barabara ya Msimbazi kuanzia Faya hadi eneo la Kariakoo-Gerezani na sehemu ya Barabara ya Kawawa kuanzia Magomeni hadi njia panda ya Morocco.
Akizungumzia utaratibu huo mpya, Ofisa Mkuu Mtendaji wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART),  Asteria Mlambo alisema magari yote, yatakayotumia mfumo wa njia hizo mpya, hayatatakiwa kuzidi mwendo wa kilometa 50 kwa saa.
Alisema utaratibu huo, unaotarajiwa kuanza hivi karibuni na kusimamiwa na  mamlaka mbalimbali, ikiwemo Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, mwendo huo usiozidi kilometa 50 utazingatiwa hasa katika barabara ya Morogoro, ambayo mradi huo unakaribia kukamilika.
Chini ya utaratibu huo mpya, pia magari hasa daladala, hayataruhusiwa kusimama njiani na pia itakuwa marufuku kufanya biashara ndogo au biashara ya aina yoyote katika maeneo ya njia hizo.
“Kwa sasa tunaangalia maeneo ya muda ambayo daladala zitaruhusiwa kusimama,” alisema Mlambo na kuongeza kuwa taratibu zote zimekamilika na kwamba  polisi wataanza kuhakikisha kuwa utaratibu huo, unafuatwa hivi karibuni.
Vyombo vingine vitakavyosimamia utekelezaji wa utaratibu huo licha ya Dart na Polisi, ni Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) na Wakala wa Barabara (Tanroads). 
Kwa mujibu wa ofisa huyo wa Dart, kuegesha magari au kufanya biashara katika maeneo ya waenda kwa miguu, hakutaruhusiwa na watakaokiuka, watapewa adhabu kali.
 “Napenda pia kuwataarifu wafanyabiashara kuacha kupaki magari ya mizigo katika njia kuu na kupakua au kupakia mizigo,” alisisitiza.
Wakati yapo mazoea ya madereva wa bajaji na pikipiki, kuegesha vyombo vyao katika njia za watembea kwa miguu, Mlambo alisema vyombo hivyo havitaruhusiwa tena kupita katika njia za waenda kwa miguu.
“Makosa yatahusisha adhabu kali na faini ya pesa taslimu,” alisema.
Alisisitiza utaratibu huo utakapoanza, kila anayehusika hasa madereva katika jiji hilo kubwa la biashara, watatakiwa kuuheshimu na kuufuata.
Mradi unaoendelea wa mabasi yaendayo haraka katika Jiji la Dar es Salaam, unalenga kuimarisha huduma za usafiri na kuwa za kisasa zaidi na kupunguza msongamano, ambao umekuwepo kwa kipindi kirefu sasa.
“Tunatarajia utaratibu huu kuanza hivi karibuni,” Mlambo aliwaambia waandishi wa habari.

No comments: