Kampuni ya Dangote Group inayomilikiwa na bilionea
kutoka Nigeria, imetangaza neema itakayotokana na uwekezaji wa kiwanda cha
saruji unaofanyika mkoani Mtwara, miongoni mwake ikiwa ni kupungua kwa
bei ya saruji uzalishaji utakapoanza.
Rais wa kampuni hiyo, Aliko Dangote, alisema
kiwanda cha Saruji cha Dangote kitakapoanza, miezi sita ijayo, licha ya
bidhaa hiyo kuuzwa kwa bei ya chini, kutakuwa na ongezeko la ajira na nafasi za
mafunzo, watachangia huduma za kijamii na uchumi kwa ujumla.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari
jana jijini Dar es Salaam, mfanyabiashara huyo alisema watatafuta njia ya
kukabili gharama zinazochangia bei ya saruji miongoni mwake, ikiwa ni kutatua
tatizo la usafirishaji wa bidhaa hiyo.
Kiwanda hicho kinajengwa kwa thamani ya dola
za Marekani milioni 500 (takribani Sh trilioni 8.3).
“Pindi kiwanda kitakapoanza kufanya kazi mwaka
ujao, tutaangalia namna ya kupunguza tatizo la bei ya saruji, siku zote kuna
nafasi ya kufanya hivyo katika uzalishaji,” alisema.
Bei ya saruji hutegemea maeneo huku usafiri
ukitajwa kuwa chanzo cha ongezeko hususani kwa mikoa ya pembezoni. Wakati
jijini Dar es Salaam, bei yake ni kati ya Sh 13,000 na 15,000, baadhi ya mikoa,
bei inazidi Sh 20,000.
Kwa mujibu wa Dangote, awali kiwanda chake
kililenga kuzalisha tani milioni 1.5 kwa mwaka lakini sasa baada ya
kukamilika, kitazalisha tani milioni tatu kwa mwaka.
Alisema kampuni imepanga kuingiza malori 250
kwa kuanzia, yatakayotumika kusambaza bidhaa hiyo nchini.
“Usafirishaji ni ghali sana kwa nchi za
Afrika Mashariki, lakini sisi tumejipanga kuingiza malori yatakayosaidia
kusambaza ingawa tutatumia na njia nyingine pia.”
Wakati huo huo , kuhusu upatikanaji wa
wafanyakazi wenye ujuzi kwa ajili ya kufanya kazi kwenye kiwanda, alisema
wamepanga kuchukua wahandisi kutoka Tanzania na kwenda kupata mafuzo ya
nadharia na vitendo katika chuo cha Dangote Academy kilichoko Abuja nchini
Nigeria.
“Kuna baadhi ya wahandisi wa kitanzania
ambao wamefanyiwa usaili kwa ajili ya kujiunga na chuo chetu na watapata nafasi
ya kujifunza kwa nadharia na vitendo kwa kufanyakazi kwenye kiwanda chetu, ili
wakirudi watumike katika uzalishaji na kuwafundisha wengine.
Alisema, “Kwa suala la ajira, theluthi mbili
ya wafanyakazi watakuwa ni Watanzania na pia kutakuwapo na wafanyakazi wageni
ambao hata hivyo hawatakaa milele, watakuwa na kazi ya kusaidia ujuzi na
kiwanda kitakapotengamaa wataondoka.”
Alipoulizwa yeye kama mmoja wa matajiri wa
Afrika, nini anachotamani kifanyike kila anapoamka, Dangote alisema nia yake ni
kuiona Afrika inapiga hatua ya juu ya maendeleo.
Akizungumza mchango wa huduma za kijamii,
Dangote alisema: “ Ingawa wajibu wa kutoa huduma kwa wananchi ni serikali,
lakini sisi tunatarajia kuchangia katika huduma ya afya, maji, shule, nafasi za
elimu na kuwajengea soko wananchi wa Mtwara.
No comments:
Post a Comment