MAJAMBAZI WAUA SISTA KANISA KATOLIKI NA KUPORA FEDHAMajambazi wamemuua kwa kumpiga risasi Mhasibu wa Kanisa Katoliki, Usharika wa Makoka,  jijini Dar es Salaam, Sista Prisencia Kapuli na kisha kumpora fedha zinazokadiriwa kuwa zaidi ya Sh milioni 10 alizokuwa nazo. 
Tukio hilo ni la jana saa 9 alasiri katika eneo la Ubungo Riverside wakati Prisencia, mtawa mwenzake pamoja na dereva wao, Mark Mwarabu, walipokwenda katika eneo  hilo  kununua mahitaji ya kanisa. 
Taarifa za mashuhuda wa tukio hilo zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, zilisema walikuwa wakitoka benki. Hata hivyo Kamanda hakutaja kiasi kilichoporwa isipokuwa inadaiwa mtawa aliyenusurika ndiye alisikika akisema. 
Inadaiwa baada ya gari lililowabeba watumishi hao wa kanisa kufika eneo hilo, Prisencia alishuka akiwa na mkoba kwenda duka la mchele na ghafla majambazi hao waliokuwa kwenye pikipiki mbili aina ya Boxer, walimvamia na kuanza kumnyang’anya mkoba wake uliokuwa na fedha hizo.
“Wakati wakiendelea kuvutana ndipo mmoja wa majambazi hao aliyekuwa akivuta mkoba huo akampiga  bastola shingoni. Hatua hiyo ilifanya auachie  mkoba na kudondoka,” alisema shuhuda na kwamba walimpiga risasi dereva kwenye kidole.  Kamanda Wambura alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea. 

No comments: