Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) vikiwa na matumaini ya kuunganisha nguvu katika uchaguzi mkuu ujao,
vimeambiwa kila kimoja kijiimarishe kivyake katika mapambano ya kisiasa.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, amesema vyama hivyo, visitegemee nguvu ya
umoja huo badala yake, vijiimarishe kuleta ushindani katika harakati zao za
kisiasa wanazoendelea kuzifanya.
Mbowe ambaye chama chake ni miongoni mwa
vinavyounda Ukawa, alisema hayo jana katika mkutano mkuu wa sita wa Chama cha
Wananchi (CUF) ambacho pia ni mwana Ukawa.
Kingine ni NCCR Mageuzi ambavyo kwa pamoja
vilifikia maafikiano ya kutoishia kwenye ushirikiano katika masuala ya katiba
mpya, bali pia masuala mengine kisiasa ikiwemo kuunda kambi rasmi ya upinzani
bungeni.
“Ni vizuri sasa wakati tupo katika
harakati hizi kupitia Ukawa, kila chama kwa nafasi yake, kikajiimarisha ili
tunapokuwa ndani ya Ukawa kila kimoja kikawa na nguvu zake hatua itakayosaidia
harakati zetu,” alisema Mbowe.
Hata hivyo Mbowe alisisitiza kwamba
ushirikiano wa vyama hivyo kupitia Ukawa, unaweza kuwa wa
umuhimu ingawa unabezwa na baadhi ya vyama.
Aliendelea kusisitiza, umoja huo siyo mapito bali
utaendelea hata suala la Katiba litakapoisha. “Umoja huu siyo mwisho wake
katika Katiba, lazima utaendelea kutuongoza mbele katika mipango mingine na
hata uchaguzi mkuu ujao hivyo wanaotubeza wajue hizo ndiyo salamu zetu,”
alisema Mbowe.
Katika mkutano mkuu huo ambao Chama Cha
Mapinduzi (CCM) pia kilialikwa na kuwakilishwa na Makamu Mwenyekiti wake, Bara,
Philip Mangula, alisema umoja waliounda ni mzuri.
Aliwaambia, “mkiwa vyama vingi dhaifu na
mkajiweka katika umoja wa pamoja ni vizuri kuliko mmoja mmoja kwa kuwa
kutasaidia kuleta upinzani. ”
Alisema hata Baba wa Taifa , Mwalimu Julius
Nyerere kipo kipindi alitamani CCM igawanyike katika makundi mawili ili
kuchagiza kukuza ushindani. Alisema ujio wa vyama vingie umesaidia kuleta upinzani
huo katika kipindi hiki.
Aidha Mangula alitaka vyama vyote kujenga
tabia ya kuvumiliana kukuza demokrasia ya kweli . Alisema kwa kufanya hivyo
kutasaidia kuondoa vurugu za kisiasa za mara kwa mara zinazojitokeza
nchini.
Mangula alipongeza CUF kwa mkutano huo
pamoja na mwaliko kwa chama chake. Pia alieleza kufurahishwa na demokrasia
ndani ya chama hicho hususani, kutokana na uwezo wake wa kukutanisha wajumbe
wake katika mkutano huo.
Alisema kufanya mkutano kama huo, ndiyo
demokrasi ya kweli. Alieleza kushangazwa na hatua ya Msajili wa Vyama vya
Siasa kuendelea kufumbia macho baadhi ya vyama ambavyo licha ya kupewa
usajili wa kudumu, havijawahi kuitisha mkutano hata mmoja.
Wakati huo huo Profesa Lipumba alitaka wajumbe
wa mkutano huo kuhakikisha wanakamilisha kikamilifu mchakato wa uchaguzi wa
kuwapata viongozi mbalimbali wa chama hicho kuepuka kuleta makundi
yatakayogharimu chama hicho siku zijazo.
Alisema wajumbe wanapaswa kutambua kuwa
uchaguzi usio na vijembe, utasaidia kukuza demokrasia ya kweli ndani ya chama
hicho wakati wakijiandaa kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment