MBUNGE AWATUPIA KIJEMBE WANAWAKE BUNGENIMbunge wa Konde, Khatibu Said Haji (CUF) amesema wanawake wameadhibiwa na Mungu katika maandiko matakatifu na kuhoji hawaoni kuwa harakati zao za kudai haki sawa, ikiwemo uwakilishi wa asilimia 50 kwa 50 katika nafasi za uamuzi kuwa ni kuingilia adhabu hiyo halali. 
 Alisema hayo bungeni jana, kwenye swali la nyongeza baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere, kuomba Serikali ipeleke muswada wa sheria bungeni,  utakaowalazimisha waajiri kuajiri wafanyakazi kwa kuzingatia asilimia 50 wanaume na asilimia 50 wanawake.
 Huku Naibu Spika, Job Ndugai, ‘akichomekea’ kuwa hoja hiyo haiungwi mkono ndio maana hakuna makofi mengi ya wabunge, Leticia alisema kwa kuwa wako wanawake wenye uwezo, elimu na makini kuliko wanaume ni vyema sheria hiyo ifikishwe bungeni, ili kuwalazimisha waajiri kuifuata.
 Akijibu hoja ya  Khatibu, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, alisema kama Mbunge wa Konde anazungumzia sheria ya dini, yeye ameisoma lakini haki za wanawake zilizopo katika sheria hiyo ya dini, zimekuwa zikidhulumiwa.
 Alitoa mfano wa haki ya mwanamke aliyeolewa kufuliwa nguo na mumewe ambayo iko katika sheria ya dini, ambayo alisema mfano unaoonesha namna haki hizo za wanawake zilizopo katika sheria ya dini, zinavyodhulumiwa.
 Baada ya kutoa jibu hilo, alisimama Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaaa (Tamisemi), Hawa Ghasia aliyesema kitabu kitakatifu cha Kurani, kimeweka wazi kuwa mwanamume ndiye mlinzi wa mwanamke na kufafanua kuwa katika hali ya kawaida, mlinzi ni mtu muhimu lakini anayelindwa ni kiongozi.
  Hata hivyo Waziri Simba katika majibu, alisema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za makusudi kutimiza lengo la uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume.
Akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge, Mbunge Haji alifafanua adhabu aliyosema wanawake wamepewa na Mungu akinukuu kitabu cha Mwanzo katika Biblia kwamba mwanamke alipewa adhabu mbili; moja ya kuzaa kwa uchungu na ya pili ya kuwa chini ya mamlaka ya mwanamume.

No comments: