Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewataka
wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania na China kutumia fursa zilizopo
katika nchi hizo kuwekeza katika sekta mbalimbali ili kuinua uchumi wao na
mataifa haya mawili.
Pamoja na hayo, Pinda alitumia fursa hiyo,
kuinadi Tanzania kuwa ni moja kati ya nchi za Afrika yenye mazingira mazuri ya
uwekezaji hasa katika sekta za kilimo, nishati, madini na utalii.
Alikuwa akizungumza katika ufunguzi wa
Kongamano la pili la biashara baina ya China na Tanzania ambalo pia
lilihudhuriwa na Makamu wa Rais wa China, Li Yuanchao, aliyeko nchini kwa ziara
ya kikazi ya takribani wiki moja.
"Napenda niwajulishe kuwa uamuzi wenu wa
kufanya biashara na Tanzania ni muafaka kwa kuwa nchi hii, mbali na kubarikiwa
rasilimali nyingi, lakini pia ina utulivu wa kisiasa, inasifika kwa amani na
ina nguvu kazi nyingi," alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Makamu huyo wa
Rais wa China akiongozana na Pinda, aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo
la Mfuko wa Mwalimu Nyerere (MNF), jijini Dar es Salaam linalojengwa na Kampuni
ya China Railway Group Limited.
Rais wa kampuni hiyo, Dai Hegen ameahidi
kwamba jengo litakuwa mradi wa daraja la juu katika menejimenti, ubora,
ufanisi, teknolojia na uzoefu. Kampuni ya China Railway Jianchang Engineering
Co. (T) Limited, ambayo ni kampuni tanzu ya China Railway Group Limited ndiyo
itakayojenga jengo hilo.
Kwa mujibu wa Rais huyo, Jengo la MNF
litajengwa katika kiwanja chenye ukubwa meta za mraba 61,000 na litakuwa na
hoteli ya nyota tano, ofisi za kiwango cha daraja la kwanza, na eneo la
maegesho.
Katika kongamano hilo, pia China na Tanzania
zilisaini mkataba wenye thamani ya dola za Marekani milioni 200 kwa ajili ya
kuisaidia Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (Dawasco) katika ujenzi wa bwawa la
Kidato, mtambo wa maji na miundombinu yake mkoani Morogoro.
No comments:
Post a Comment