MABADILIKO TABIANCHI TISHIO VISIWANI ZANZIBARMabadiliko ya tabia nchi yameathiri visiwa vya Zanzibar na kutishia ustawi wa kilimo hususani cha mpunga. 
Waziri wa Maji, Ujenzi na Nishati, Ramadhan Abdalla Shaaban alisema hayo jana akisisitiza kwamba kilimo cha kutegemea mvua kimeathirika kwa kiwango kikubwa na mapato ya wakulima kushuka. 
Shaaban kwa niaba ya Waziri wa Kilimo na Maliasili,  alikuwa akifanya majumuisho na kujibu hoja mbali mbali za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi  waliochangia bajeti ya wizara  hiyo kwa mwaka wa fedha 2014-2015.
Alisema maeneo mengi ya kisiwa cha Unguja na Pemba yameathirika kwa kuingia maji ya chumvi katika mabonde. Kwa mujibu wake,  zaidi ya maeneo 30 yameathirika kwa kuingiwa na maji ya chumvi kisiwani Pemba, wakati kwa upande wa Unguja maeneo 20 yameathirika.
“Kilimo cha mpunga kwa sasa kinakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo maji ya chumvi kuvamia mabonde ya wakulima na kuacha moja kwa moja kilimo hicho,” alisema.
Mwakilishi wa  Mtambwe, Salim Abdalla Hamadi (CUF) alitaka serikali kuchukua hatua za haraka kukabili  mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo athari zake katika sekta ya kilimo ni kubwa.
Alitoa mfano wa jimbo lake, zaidi ya maeneo sita yameathirika na kazi za kilimo zimesita kutokana na mwingiliano huo wa maji ya chumvi. 
“Tunaiomba Wizara ya Kilimo na Maliasili kutusaidia kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabia ya nchi,” alisema Hamadi. 
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamepitisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya  wizara hiyo iliyoomba kuidhinishiwa Sh 13,758,000,000 kwa kazi za kawaida, mwaka wa fedha 2014/15.

No comments: