KIINI CHA GRIDI YA TAIFA KUZIMIKA GHAFLA BADO KITENDAWILI

Shirika  la Umeme  Tanzania (TANESCO) bado halijajua sababu ya umeme kuzimika nchi nzima juzi usiku, baada ya gridi ya taifa kuzimika ghafla.
Limeeleza kuwa wanafanyia kazi taarifa zilizorekodiwa na Kituo cha Kudhibiti Mifumo cha Ubungo ili kujua chanzo cha kuzima kwa gridi hiyo.
Hayo yalisemwa  jana na Kaimu Meneja Uhusiano Tanesco, Adrian Severin.
Alifafanua kuwa kitendo hicho, wanakichukulia ni dharura ambacho ni nadra kutokea  kwa gridi yote kuzima.
Alisema umeme ulikatika juzi  saa 1.19 usiku  baada ya gridi ya taifa, kuzima na hivyo kusabisha nchi nzima kukosa umeme na kurejea saa 4:48 usiku nchi nzima, baada ya kuwasha mashine zote bila tatizo kuonekana.
Alisema  kutoka kwa gridi ya taifa, kuna sababu mbili kuu, moja kama kukitokea hitilafu ya mmoja ya mitambo ya kuzalisha umeme mfano Kidatu, Mtera, Kihansi, Hale, New Pangani, Nyumba ya Mungu, Ubungo 1 & 2 au Tegeta gridi inaweza kuzima.
“Yaani kwa lugha rahisi ni kwamba mitambo yote ya kuzalisha umeme, inabeba mzigo mmoja, kama mtambo mmoja ukizima , unasababisha ombwe  ambapo mitambo inayobaki inashindwa kuubeba na hivyo nayo kuachia mzigo na hatimaye mashine zote hutoka (huzima),”alisema.
Severin alisema sababu ya pili, mitambo ya wateja wakubwa kama vile migodi na viwanda vikubwa vya uzalishaji, wateja hao wakubwa mitambo yao ikipata hitilafu na kuzima ghafla, inaweza kusababisha mfumo wa gridi kuzima kwa mtindo huo huo wa kuzidiwa kwa mzigo kwa mitambo.
Alisema kwa nchi nyingine,  gridi haiwezi kuzima kwa kuwa wanazalisha umeme wa ziada, kama vile kwa kutumia makaa ya mawe ambapo ukishauwasha huwezi kuuzima, hivyo wana umeme ambao uko 'standby', ukipungua tu kwenye gridi, basi umeme wa akiba unaziba hilo ombwe.

No comments: