JAJI MIHAYO ACHAGULIWA RAIS MPYA WA BARAZA LA HABARI

Mkutano wa kumi na saba wa wanachama wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) umemchagua Jaji mstaafu Thomas Mihayo kuwa Rais Mpya wa Baraza hilo kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Baraza hilo lililoketi mjini Bagamoyo mkoani Pwani, pia limemchagua Hassan Abdallah Mitawi, Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kuwa Makamu wa Rais kwa baraza hilo.
Rias mpya  wa MCT, Jaji Mihayo amechukua nafasi hiyo kutoka kwa Jaji mstaafu Robert Kisanga, ambaye muda wake wa kutumikia baraza hilo kikatiba umemalizika.
Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa Uchaguzi huo, Jane Mihanji alisema uchaguzi huo umewarejesha kwenye Bodi hiyo ya MCT, Badra Masoud ambaye ni Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini  na Rose Haji, ambaye ni mwandishi  mkongwe, kuendelea na wadhifa wao.
Kulingana na Katiba ya MCT,  wajumbe wawili wa Bodi hiyo wanaomaaliza muda wao, wanaruhusiwa kuchaguliwa tena, kuendelea na wadhifa huo kwa kipindi kingine.
Wajumbe wapya waliochaguliwa kujiunga na bodi hiyo kutoka kundi la waandishi wa habari ni  Tuma Abdallah, ambaye ni Mhariri wa gazeti la Daily News na Wallace Maugo, ambaye ni Mhariri wa gazeti la The Guardian.
Kutoka kwemye kundi la jamii, waliochaguliwa kwenye bodi hiyo ni Profesa Bernadetha Killian, ambaye ni  Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa cha Chuo Kikuu cha Dar es Saalam na Ali Mfuruki ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Mwananchi inayofanya biashara hapa nchini kwa jina la ZUKU na Jaji mstaafu, Juston Mlay.

No comments: