MOROGORO KUACHANA NA ANALOJIA JUNI 30

Mamlaka ya  Mawasiliano Tanzania (TCRA) inatarajia kuzima mitambo ya kurusha  matangazo kwa mfumo wa utangazaji wa analojia mkoani hapa ifikapo Juni 30, mwaka huu saa sita usiku.
Hayo yalibainishwa jana na Albert Mwanjesa wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema kuwa vigezo vitakavyotumika kuzima mitambo ya analojia ni pamoja na kuwepo kwa utangazaji wa mfumo wa analojia pamoja na digitali.
Mwanjesa alisema kutakuwepo upatikanaji wa visimbusi na uwepo wa chaneli tano za kitaifa kwenye mfumo wa kidijiti ambazo ni TBC1, ITV, Channel Ten, Star Tv na EATV.
Alizitaja chaneli ambazo bado ziko kwenye mfumo wa analojia kwa Mkoa wa Morogoro kuwa ni pamoja na televisheni za Sua, Star, Channel Ten na Abood.
 Hata hivyo alisema  elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali kuhusu kuhamia katika teknolojia ya mfumo wa utangazaji wa dijitali imekuwa ikitolewa kwa kiwango cha kuridhisha  na kwamba imewafikia wananchi kwa asilimia zaidi ya 22 kati ya asilimia 24 wanaopata matangazo ya televisheni  ya analojia.
Aidha alisema kuwa  utaratibu wa kuzima mitambo ya analojia utakuwa kwa maeneo yenye matangazo ya dijitali pekee na kwamba katika maeneo ambayo hayana miundombinu ya dijitali hayatazimwa kwa sasa hadi yapate mfumo huo.
Naye Mhandisi wa Mamlaka hiyo, Christopher Assenga akizungumzia tatizo la kuganda kwa picha ambalo limekuwa kero kwa wananchi walio wengi alisema kuwa wataondoa tatizo hilo kwa kujenga mitambo midogo kwenye maeneo ambayo matangazo hayo hayapatikani vizuri.

No comments: