CHAMA CHA CUF CHAFANYA MABADILIKO MAKUBWA

Mkutano Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) umeridhia uwepo wa ngazi ya uongozi wa jimbo, ili ufanane na mfumo wa vyama vingine vya upinzani nchini, kwa lengo la kuimarisha mshikamano.
Pia, mkutano huo umekataa pendekezo la kuwepo ngazi ya uongozi ya mkoa, huku kikieleza kuwa mapendekezo hayo, hayawezekani kwa kuwa chama hakina uwezo wa kuendesha ngazi hiyo.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuelezea mambo yaliyojiri juzi kwenye mkutano huo unaoendelea.
Kambaya alisema katika mkutano huo,mapendekezo mawili ya marekebisho ya katiba ya CUF, yaliwasilishwa na Baraza Kuu la uongozi la chama hicho.
Mapendekezo hayo ni kutaka kuwepo na ngazi za uongozi ya mkoa na jimbo, kama ambavyo vyama vingine vya upinzani vya Chadema na NCCR-Mageuzi walivyo.
Alisema lengo la mapendekezo hayo ni kutaka kuwa na mfumo wa uongozi, unaofanana hasa baada ya vyama hivyo kuwa na ushirikiano wa karibu na kutaka kuimarisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Alisema baada ya mkutano mkuu kupokea mapendekezo hayo, ulikubali pendekeo moja la uwepo wa ngazi ya uongozi ya jimbo na kukataa ya mkoa.
Kambaya alisema baada ya mkutano mkuu kutoridhia pendekezo hilo, wanachosubiri sasa ni Baraza Kuu kukaa na kutoa mwongozo wa nini cha kufanya, ili waweze kwenda sambamba na wenzao kwenye vikao.
Pendekezo lingine lilikuwa ni kubadilisha mfumo wa uchaguzi wa makatibu wa wilaya wa chama hicho, wawe wanateuliwa na kamati ya utendaji ya taifa ya CUF.
Hata hivyo, pendekezo hilo lilikataliwa kwa mkutano huo kusema halina mantiki na hivyo mfumo wa awali wa kuwachagua kwa kura, utaendelea.
Katika hatua nyingine, chama hicho kimeunda Kamati ya Maadili na Nidhamu ambayo sasa itakuwa inatambulika rasmi kikatiba na chama hicho.
Kamati hiyo itaongozwa na wajumbe sita na itaongozwa na Makamu Mwenyekiti Taifa wa CUF.
Pamoja na mambo hayo, chama hicho jana jioni kilifanya uchaguzi wa viongozi wakuu wa chama, ikiwepo nafasi ya mwenyekiti, makamu mwenyekiti na katibu.
Nafasi ya Mwenyekiti inawaniwa na wajumbe watatu, ambao ni Profesa Ibrahim Lipumba, Adam M'bezi na Chief Jemba.
Nafasi ya Makamu inawaniwa na  watu wawili ambao ni Juma Duni Haji na Haji Kombo. Nafasi ya Katibu inawaniwa na mgombea mmoja, Maalim Seif.

No comments: